WAKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kutoka
nchi 25 barani Afrika, wametakiwa kutumia vizuri mafunzo ya operesheni za
pamoja ili kukabiliana na uhalifu.
Uhalifu huo ni pamoja na vitendo vya ugaidi na uhamiaji haramu
ambavyo vinajitokeza kwa kasi katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa
Afrika.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, DCI
Robert Manumba, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari
baada ya kufungua Mafunzo ya
Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai.
Washiriki wa mafunzo hayo ni kutoka
Umoja wa Wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) na Umoja wa Wakuu wa
Polisi Afrika Mashariki (EAPCCO).
Lengo la mafunzo hayo ni kufanya
operesheni za pamoja ili kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.
DCI Manumba alisema, uhalifu
unaofanyika nchini na ukanda wa Afrika Mashariki ndio huo huo unaotokea katika
nchi nyingine hivyo kunahitajika ushirikiano na kubadilishana taarifa ambazo
zitasaidia kutambua na kuweka mikakati thabiti ya kudumisha amani na usalama
barani Afrika.
“Kwa mfano, suala la wahamiaji
haramu hatuwezi kupambana nalo sisi wenyewe...wahamiaji hawa wanatoka nchi
nyingine na hapa wanapita tu kwenda katika nchi tofauti hivyo lazima
tubadilishane taarifa, kuwa na mkakati wa pamoja ili kuwabaini wanaofanya
vitendo hivi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi wa
Kimataifa (Interpol), Kanda ya Afrika Mashariki kutoka nchini Kenya, Bw. Rego
Francis, alisema Jeshi la Polisi katika nchi husika zina wajibu wa kutoa elimu
ya kutosha kwa wananchi.
Alisema elimu hiyo itawawezesha
kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya usalama mapema ili ziweze kufanyiwa
kazi haraka kabla matukio hayajatokea.
Mkuu wa Kitengo cha Interpol nchini,
Kamishna Msaidizi wa Polisi Gustavus Babile, alisema lengo la mafunzo hayo ya
siku mbili ni kubadilishana uzoefu, kupeana mbinu, kuweka mikakati ya kufanya
operesheni zitakazoweza kuutokomeza uhalifu.
Alisema kupitia mafunzo hayo
wataweza kuandaa operesheni zenye mafanikio ambazo zitaweza kushirikisha nchi
nyingi ili kukabiliana na ugaidi, dawa za kulevya, wahamiaji haramu, wizi wa
magari na uhalifu wa aina nyingine unaotokea barani Afrika.
Mafunzo
hayo yanafanyika baada ya kumalizika mkutano wa 18 wa Wakuu wa Polisi Kusini
mwa Afrika (SARPCCO), ambao waliazimia kufanya operesheni za pamoja.
No comments:
Post a Comment