CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeitaka Serikali itoe tamko
la kuiomba radhi Serikali ya Saudi Arabia kutokana na raia wake wanne
kuhusishwa na tukio la ulipuaji bomu mkoani Arusha na baadaye kuachiwa baada ya
uchunguzi kubaini hawakuhusika.
Tukio hilo
lililotokea Mei 5 mwaka huu, katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, mkoani humo ambapo watu watatu walifariki dunia
na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Mwenyekiti wa
chama hicho Taifa,
Prodesa Ibrahim Lipumba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana
wakati akifungua Kikao cha Baraza Kuu la chama hicho na kuongeza kuwa, kwa muda
mrefu Saudi Arabia na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri hivyo ni wajibu wa
Serikali kuomba radhi ili kuendeleza uhusiano huo.
Alisema wageni hao waliingia nchini
kihalali hivyo kitendo cha kuhusishwa na tukio hilo ambalo limetangazwa katika
vyombo mbalimbali vya habari kimechafua jina la nchi yao.
“Serikali inapaswa kuwa makini na
inachokifanya, kitendo cha kuwakamata wageni hawa ambao wanatoka kwenye nchi ya
Kiislamu, kinaweza kuwagawa Waislamu na Wakristo kitu ambacho ni hatari kwa
Taifa,” alisema.
Aliongeza kuwa, Serikali inatakiwa
kuchukua hatua stahiki yanapotokea matukio makubwa kama hilo la uvunjifu wa
amani ili kuwajengea imani Watanzania kuwa Serikali yao ipo makini.
Katika hatua nyingine, Prof. Lipumba
alizungumzia uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, kumuachia huru Katibu
wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda.
Alisema kilichofanywa kwa kiongozi
huyo si cha kiungwana kwani kesi iliyokuwa ikimkabili ilikuwa ikihusu kiwanja
hivyo ingehamishiwa kwenye Mahakama ya Ardhi.
“Serikali imekuwa ikikuza mambo na
kusababisha mifarakano katika jamii...inapaswa kufanya uchunguzi wa kina kwanza
kwani mwisho wa siku nchi itaingia katika matatizo,” alisema.
Pia Prof. Lipumba alidai kuhofia
deni kubwa la Taifa na kudai kuwa ili kuondokana na madeni ya aina hiyo,
Serikali inapaswa kuacha tabia ya kukopa bila utaratibu kwani mwisho wa siku
tutashuhudia Taifa likipata mzigo wa kurejesha madeni hayo.
Aliongeza kuwa, kipindi cha utawala
wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa, wakati akiingia
madarakani alikuta Taifa likiwa na deni kubwa hivyo alitumia kipindi cha miaka
mitano kulipunguza sana.
Alisema pamoja na nchi kuwa na
rasilimali za kutosha katika Taifa, bado utegemezi umekuwa mkubwa na Serikali
imekuwa bingwa wa kutoa ahadi za
kutekeleza miradi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment