02 April 2013

Watendaji wa serikali lawamani kwa rushwa


Na Florah Temba,
Moshi.

TATIZO la uharibifu wa mazingira katika Mkoa wa Kilimanjaro, limeelezewa kuendelea kushika kasi kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali kujiingiza kwenye vitendo vya Rushwa na kuvifumbia macho vitendo vya uvunaji miti na upasuaji wa mbao.

Hayo yalibainishwa na Ofisa Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rishwa (TAKUKURU) mkoani Kilimanjaro,Bw.Benedict Mongella, wakati akizungumza na watendaji wa kata,maofisa
tarafa na wakuu wa idara mbalimbali katika  Halmashauri ya wilaya ya Moshi mkoani hapa, ambapo alisema ili kumaliza tatizo la uharibifu wa mazingira ni lazima watendaji wakabadilika na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Alisema kumekuwepo na baadhi ya watumishi wa umma ambao wamekuwa wakizitumia ofisi za umma na madaraka yao vibaya na kushindwa kutekeleza
wajibu wao,hali ambayo inasababisha kuendelea kukithiri kwa vitendo vya uharibifu wa mazingira.

Aidha Bw. Mongella alisema,katika ufuatiliaji wao wamebaini kuwa wapo baadhi ya watendaji wa vijiji na kata, ambao wamekuwa wakipokea rushwa na
kushirikiana na wafanyabiashara kusafirisha mazao ya misitu kinyume cha sheria .

“Wapo baadhi ya watendaji ambao wamekuwa wakihusika moja kwa moja katika vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa kujiingiza kwenye vitendo vya
rushwa, na kuruhusu uharibifu kuendelea kwa kasi,kwani mnapochukua fedha za watu ni dhahiri kabisa kuwa hamtaweza kutenda haki wala kukemea vitendo vya uharibifu wa mazingira,”alisema.

Alisema tatizo la rushwa linatokana na ukosefu wa maadili kwa viongozi na tamaa ya fedha hali ambayo huwafanya kusahau majukumu yao hivyo
kuwataka kurejea katika maadili ya utawala bora.

Kufuatia hali hiyo Ofisa huyo aliwataka watendaji hao kubadilika na kutekeleza majukumu yao kwa haki na usawa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
wanasimama vema katika nafasi zao na kukemea vitendo vyote vya uharibifu wa mazingira.

“Mazingira yataendelea kuharibika kama ninyi watendaji hamtabadilika kwani baadhi ya watendaji wamekuwa wakifanya kazi kwa kutegemea rushwa,ni lazima sasa mbadilike na kuacha kutumia nafasi zenu za madaraka vibaya,”alisema.

Akizungumza Afisa maliasili mkoa wa Kilimanjaro Bw. Isaria Masam, alisema tatizo la uharibifu wa mazingira katika mkoa wa Kilimanjaro bado ni
kubwa,na kwamba zoezi la udhibiti uharibifu huo halitafanikiwa kama watendaji wa kata na vijiji hawatabadilika.





No comments:

Post a Comment