02 April 2013

Wananchi watumia mitishamba kujitibu


Na Joseph Mwambije,
Songea

KUTOKUWEPO kwa Zahanati na miundombinu mizuri ya barabara katika kijiji cha Magwamila ambacho kiko mpakani na nchi ya Msumbiji katika kata ya Muhukuru Songea vijijini mkoani Ruvuma kumewalazimisha wananchi kujitibu kwa kutumia mitishamba.

Hayo yalielezwa juzi na diwani wa Kata ya Muhukuru Bi.Agatha Gama wakati akizungumza kwenye Kikao cha Baraza la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Songea kilichofanyika mjini Songea.

Alisema kuwa kukosekana kwa Zahanati na barabara kunawafanya wananchi wa kijiji hicho kuishi maisha ya zama za kale kwa kujitibu kwa mitishamba na kuitaka Halmashauri hiyo kutengeneza barabara za Kata yake na kupeleka dawa kwenye Zahanati
ya kijiji hicho iliyokamilika hivi karibuni ambayo haijaanza kutumika.

"Kijiji cha Magwamila toka kianzishwe hakijawahi kupelekewa huduma za msingi,hivyo wananchi wake wanajiona kuwa wao si sehemu ya Watanzania naiomba
Halmashauri kupeleka huduma hizo haraka ili na wao wajione ni sehemu ya Watanzania,"alisema.

Hata hivyo diwani huyo alisema kuwa wananchi hao
watashangaa Zahanati iliyojengwa hapo na dawa zinavyotolewa kwa upande wa vidonge na sindano kwa kuwa wao walikuwa wakitibiwa na mitishamba tuu na siyo vinginevyo.

Aliongeza kuwa hata  njia wanazo zitumia wananchi wa kijiji hicho zilikuwa ni mapito ya wanyama kama tembo na kuitaka Halmashauri hiyo kuharakisha ujenzi wa barabara haraka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo  Bw. Rajabu Mtiula alisema kuwa Halmashauri yake imejipanga kupeleka huduma za msingi kikiwemo kijiji hicho katika maeneo ya pembezoni.No comments:

Post a Comment