02 April 2013

Watembea kilometa 10 kufuata matibabu


Na Martha Fataely,
Same

WAKAZI wa kata ya Mpinji wilayani Same, hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 10 huku wakiwa wamewabeba wagonjwa kwa kutumia machela na vitanda kuwapeleka hospitali ya jirani ya kata hiyo, kufuatia kata hiyo kukosa zahanati.

Diwani wa viti maalum kata hiyo,Namkunda Izungo alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kata hiyo kwa shughuli za maendeleo ya wananchi.

Alisema wananchi hulazimika kutumia zahanati iliyopo kata ya Myamba au kituo cha afya kinachomilikiwa na kanisa katoliki kata ya Bwambo
wilayani humo ambavyo kwa pamoja vipo mbali na makazi ya wananchi wa kata yake.

“Wananchi wa kata hii hususani wanawake wajawazito na watoto hupata wakati mgumu mara wanapougua, kwani zahanati ipo mbali na makazi yetu….tatizo huwa kubwa zaidi, iwapo kutakuwa na mgonjwa nyakati za usiku,”alisema.

Diwani Izungo alisema pamoja na kukosa zahanati, lakini pia hakuna gari la wagonjwa ambalo linaweza kutoa huduma za haraka za kuwapaleka wagonjwa katika kata hizo za jirani au hospitali ya Wilaya iliyopo Same mjini.

“Wananchi wametengewa eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na tayari wamekusanya mawe ya kutosha kuanza ujenzi,tunahitaji kusaidia na wananchi wazaliwa wa kata hii waishio mikoa mbalimbali nchini na viongozi kwa ujumla,”alisema.

Mmoja wa wananchi wa kata hiyo,Mary Msofe alisema pia kata inakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara, ambazo hazipitiki nyakati zote za
mwaka na hivyo kuwawia vigumu kupata hata magari ya kubeba wagonjwa.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa kata hiyo,Emanuel Macha alithibitisha madai ya diwani na wananchi hao na kuongeza kuwa tayari taarifa hizo zimefikishwa halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya kulipatia
ufumbuzi wa kudumu.



No comments:

Post a Comment