02 April 2013

Waachieni watoto urithi wa elimu siyo mali-Bulembo


Na Mwandishi Wetu,Singida

WANANCHI wameaswa kuwaachia watoto wao urithi wa elimu badala ya mali ili waweze kukabiliana na changamoto za sasa za sayansi na teknolojia.

Wito huo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Taifa Abdallah Bulembo wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mangida baada ya kuzindua shule ya Chekechea kijijini hapo Wilayani Singida.

“Ndugu zangu, nataka niwaambie ukweli kwamba suala la elimu halina mbadala. Kila mzazi anawajibu na kuhakikisha kwamba watoto wake wanakwenda shule tena kwa wakati muafaka.

“Katika karne hii mtoto anatakiwa kupewa urithi wa elimu na si mali kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma kwani kufanya hivyo ni sawa na kumchimbia kaburi mtoto wako,” alisema Bulembo.

Alisema kwa kipindi kirefu sasa serikali imekuwa ikitilia mkazo suala la elimu kwa wananchi wake kwa kuboresha huduma zake mbalimbali.

Kwa mujibu wa Bulembo, katika kitilia mkazo suala la elimu, serikali katika kipindi hiki imeajiri zaidi ya walimu 25 elfu kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu shuleni.

“Kila mtu anajua kwamba tuna uhaba wa walimu katika shule zetu za msingi na sekondari, lakini serikali yetu iko makini ana imejipanga kulishughulikia suala hilo na mpaka dakika hii, tayari walimu hao wameshasambazwa katika vituo vyao vya kazi na shule za vijijini zimepewa kipaumbele zaidi,” alisema.

Mwenyekiti huyo pia alisema jumuia yake haiku nyuma katika kusimamia malezi bora na kuotoa elimu yenye kiiwango inayokidhi haja kwa jamii.

Alisema kutokana na uwingi wa shule za msingi na sekondari, jumuia hiyo sasa imebuni mkakati wa kujenga vyuo vya ufundi ili kusaidia wanafunzi wanaofeli kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

Bulembo alisema vyuo hivyo vitakuwa mkombozi wa kudumu kwa wanafunzi hao ambao wangeweza kuzagaa mitaani baada ya kufeli kwao.

“Vyuo hivi ni dawa mbadala kwa watoto wetu wanafeli katika shule za ,msingi na wale wa kidapo cha nne. Sisi katika vyuo hivi hatutaangalia maksi za mtoto anayetaka kujiunga nasi…hata kama kapata ziro tutamchukua na akimaliza chuo atakuwa mfano wa kuigwa kwa wengine,” alitamba Bulembo.

Bulembo alisema vyuo hivyo vya ufundi vitakuwa na walimu wazuri wenye uelewa na taaluma zao na hivyo kuwa sehemu ya kimbilio kwa jamii.

No comments:

Post a Comment