04 April 2013

Wanaofanya ibada mbaya kwa JK waonywa


Na Mwandishi Wetu, Mbeya

VIONGOZI wa dizi zote nchini, wametakiwa kuacha mara moja kutoa matamko ya laana na kufanya ibada za kumuombea mabaya kiongozi wa nchi Rais Jakaya Kikwete, kwani kufanya hivyo ni kusababisha Taifa na Watanzania wote kupata laana na ndio
sababu ya kutokea majanga mengi siku hadi siku.

Onyo hili limetolewa juzi na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste nchini, William Mwamalanga wakati akifunga Kongamanao la Pasaka, mkoani Mbeya.

Alisema kongamano hilo lilishirikisha vijana 2,000 na kuongeza kuwa, chanzo cha mabalaa yanayolikumba Taifa yanachangiwa
na matamko mabaya ya viongozi wa dini kwa Serikali na kuacha
wajibu wao wa kuonya, kukemea dhambi na machukizo kwenye jamii kama biashara ya dawa za kulevya.

“Rais wa nchi huapa kuilinda ardhi na watu wake, nawasihi
vijana lindeni vinywa vyenu na unafiki na hasa wa kisiasa
kwani imeandikwa usilaani wala usihukumu.

“Misikiti iliyomsomea Rais Kikwete na viongozi wengine itikafu
ya kifo, wamejilaani wenyewe na watoto wao...dua la kuku kamwe halimpati mwewe ambaye ameamliwa kumtawala kuku,” alisema.

Mchungaji Mwamalanga aliwahoji Maaskofu waliohudhuria kongamano hilo ni mafanikio gani yamefikiwa kutokana na
matamko yaliyotolewa zaidi ya kuzidisha mabalaa kila kukicha.

Alionesha kukerwa na lugha ya uchochezi iliyotolewa na Askofu
mmoja kutoka mkoani Iringa ambaye aliwataka vijana watumie nguvu zao kujitawala.

“Nawaomba vijana mpendane bila kujali itikadi na dini zenu, msikubali kutumiwa kama nguo za kupigia deki na wanasiasa
ambao mara zote huyafanya hayo kwa masilahi yao,” alisema.

Alisema umefika wakati wa vijana kuwakimbia viongozi wa dini
au wanasiasa wachochezi badala yake wahubiri amani, kuonesha uzalendo, kujiamini na kulipenda Taifa lao.

“Iwazeni Tanzania yenu na kulilinda, wanasiasa wasiwatumie vibaya mkachukian wenyewe kwa wenyewe bali mnapaswa
kufanya kazi pamoja ili kujiletea maendeleo,” alisema.

Akizungumzia malumbano ya dini nchini. Mchungaji Mwamalanga alisema Katiba ya nchi inatamka wazi kuwa, nchi haina dini hata Mwenyezi Mungu hana dini bali yeye ni mtakatigu.

“Maandiko matakatifu yanasema, mtakuwa watakatifu kama yeye, hasemi mtakuwa na dini kama alivyo na dini...huu mvutano wa nani mwenye haki ya kuchinja, wanaoukuza ni viongozi wa Serikali wasioelewa kwani kuchinja ni ibada.

“Ni vyema Serikali ibaki na kazi ya kitaalamu yaani kukagua nyama na kila imani ijichinjie yenyewe, Ijumaa Waislamu wanakwenda msikitini na Wakristo huenda kwenye ibada Jumapili mbona
hawagombani,” alisema Mchungaji Mwamalanga.

Aliongeza kuwa, Rais Kikwete amefanya kazi kubwa ya kuimarisha michezo nchini kama njia moja wapo ya kuwalinda vijana na maambukizi ya UKIMWI na kukuza vipaji vyao ambapo hivi
sasa Taifa lipo juu kimichezo.

2 comments:

  1. SIAMINI KWAMBA MAJANGA YANASABABISHWA NA KUMUOMBEA MABAYA RAIS WA NCHI.NAWEZA TU KUAMINI KWAMBA UOVU UMEZIDI NA KIKOMBE KIMEFURIKA.MAANA HAKUNA MAANDIKO MATAKATIFU YANAYOSEMA KWAMBA UKIMWOMBEA MABAYA RAIS WA NCHI,MAJANGA YATAIPATA NCHI.ILA UOVU NDIO MOJA YA NJIA ZA KUKARIBISHA MAJANGA. HATA HIVYO KAMA RAIS ANAISHI MAISHA MATAKATIFU DUA ZOTE MBAYA HAZIWEZI KUMDHURU HATA KIDOGO,MAANA ULINZI WA MUNGU UTAKUWA JUU YAKE.

    ReplyDelete
  2. ACHA UNAFIKI MCHUNGAJI FANYA KAZI YA BWANA KWA MISINGI YA KWELI WALA USIOJITAFUTIE UMAARUFU KATIKA KIPINDI HIKI CHA MPITO. THINGS ARE OPEN IF YOUR A GOOD FOLLOWER

    ReplyDelete