04 April 2013

Uchunguzi kuporomoka ghorofa Dar, vifo 13 mgodini waendelea


Na Stella Aron

JESHI la Polisi nchini, linaendelea kufanya uchunguzi wa matukio ya kuanguka kwa ghorofa 16 katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuanguka kwa kifusi katika machimbo ya Moshono, mkoani
Arusha ili wahusika wahusika waweze kuchukuliwa hatua.


Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari Dar es Salaam na Msemaji wa jeshi hilo Makao Makuu, Bi. Advera Senso, alisema matukio yote yalisababisha vifo, majeruhi na uhalibifu wa mali hivyo polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo.

“Jeshi la Polisi linawashukuru wananchi wote, vikundi vya ulinzi shirikishi vya mitaa na vijiji pote nchini, madhehebu ya dini na kampuni binafsi za ulinzi kwa kuimarisha usalama wa raia na
mali zao katika maeneo mbalimbali kipindi chote kuanzia
mkesha wa Pasaka hadi sikukuu yenyewe,” alisema.

Aliongeza kuwa, takwimu za uhalifu nchini zinaonesha kuwa, kipindi chote cha Sikukuu ya Pasaka hakukuwa na uhalifu
mkubwa ambapo viashiria vilivyojitokeza viliweza
kudhibitiwa kwa kushirikiana na wananchi.

“Ubia huu unaonyesha mafanikio ya dhana ya Polisi Jamii na
Ulinzi Shirikishi kwa vitendo...tunawapongeza wananchi wote
kwa kupuuza ujumbe wa vitisho uliotumwa katika siku zao za
mkononi (sms), na baadhi ya watu ili kuwatia hofu washindwe kuendelea na shughuli zao,” alisema.


Aliwataka wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kuimarisha ulinzi, usalama wa raia na mali zao kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu mapema kabla haujatendeka, kuzingatia ushauri wa namna ya kujilinda na kuzuia vyanzo vya uhalifu katika maeneo ya makazi na sehemu nyinginezo.

1 comment:

  1. Kuporomoka kwa jengo Dar ni matokeo ya mfumo wa kiufisadi ulioota mizizi nchini kwetu. Kutokana na hali hii mtu anaweza kufanya chochote kwa kutumia rushwa. Hakuna jipya hapa.

    ReplyDelete