04 April 2013

Serikali isikilize kilio cha Nkamia jimboni kwake


APRILI 2 mwaka huu, Mbunge wa Kondoa Kusini, mkoani Dodoma, Bw. Juma Nkamia (CCM), alizungumza na waandishi
wa habari ili kufikisha kilio chake serikalini juu ya tatizo la njaa ambalo linawakabili wapiga kura wake.

Katika maelezo yake, Bw. Nkamia alisema tatizo hilo limesababisha baadhi ya wananchi jimboni humo kula mizizi baada ya Serikali kushindwa kupeleka chakula cha msaada.

Alisema tatizo hilo lilianza Desemba 2012 hasa katika kata za Kwa Mtoro, Farukwa, Goma na Mondo ambapo juhudi zake za kuomba chakula serikalini, bado zimeendelea kugonga mwamba.

Bw. Nkamia aliongeza kuwa, alishazungumza na Waziri Mkuu,
Bw. Mizengo Pinda pamoja na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ili waweze kumsaidia chakula cha msaada lakini hadi
sasa, hakuna msaada wowote aliopewa.

Juhuzi alizofanya kama mbunge wa jimbo hilo kwa kutumia mshahara wake ili kunusuru maisha ya wananchi jimboni humo, zimepunguza tatizo hilo kwa kiwango kidogo hivyo hali hiyo inamuweka katika mazingira magumu na wapiga kura wake.

Sisi tunasema kuwa, Bw. Nkamia hana tofauti na wabunge
wengine waliopewa nafasi za uwaziri ambao wakifikisha kero
zao katika taasisi mbalimbali zinazohusika na maafa ya aina
hiyo, wanatekelezewa shida zao kwa wakati bila kuchelewa.

Mara nyingi tumepata kusikia kauli ya kiongozi wa nchi akisema, pamoja na tatizo la uhaba wa mvua ambazo zimechangia mavuno kuwa kidogo, hakuna mwananchi ambaye atakufa na njaa.

Imani yetu ni kwamba, alichokisema Rais Jakaya Kikwete ni matokeo ya Taifa kuwa na akiba ya chakula cha kutosha sasa
iweze leo hii Bw. Nkambia anyimwe msaada na kusababisha
wapiga kura wake wale mizizi.

Kitendo cha Bw. Nkamia kufikisha kilio hicho kwa waandishi,
ni wazi kimetokana na machungu aliyonayo kwa Serikali ya
chama tawala yenye jukumu la kutekeleza maagizo ya Rais
Kikwete wakati akiwatoa hofu Watanzania.

Ni jambo la kusikitisha kwa wananchi wa Jimbo la Kondoa
Kusini, kuachwa kama yatima wasioa na baba wala mama
wakati Serikali inatambua wajibu wake ili kuondokana na
aibu tunayoipata kwenye nchi jirani zilizotuzunguka.

Tanzania ni nchi ambayo hutegemea kilimo kukuza uchumi
wake na inasifika kwa kuzalisha mazao mengi ya chakula na
biashara hivyo hatutegemea kama Serikali itaendelea kukaa
kimya bila kusikiliza kilio cha Bw. Nkamia.

Matukio kama haya, yanachangia wananchi kuichukia Serikali
inayoongoza dola wakati Taifa lina akida ya kutosha hivyo ni
wajibu wa Serikali kupeleka chakula haraka iwezekanavyo.

Upo umuhimu wa Bw. Pinda na Waziri mwenye dhamana katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwenda jimboni humo ili kuwaeleza wananchi sababu zilizochangia ombi la mbunge wao kutotekelezwa kwa wakati ili waendelee kuwa na imani naye.

No comments:

Post a Comment