02 April 2013

Wanafunzi Bagamoyo walalamika kubakwa



Na John Gagarini, Bagamoyo

WATU wasiofahamika katika Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wanadaiwa kuanzisha mtandao wa kuwakamata wanafunzi wa kike, kuwabaka wanapokwenda shuleni au kurudi nyumbani.


Wakizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, baadhi ya wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Ubena, walisema mtandao huo unawahusisha Wamasai ambao wanajihusisha na
kazi ya kuchunga ng'ombe.

Walisema wachungaji hao wamekuwa wakiwavizia vichakani kwenye njia inayokwenda shuleni kwao na kuwabaka.

Kutokana na malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw.
Ahmed Kipozi, ametoa agizo la kusakwa kwa wachungaji hao
ambao wamekuwa tishio kwa wanafunzi wa shule hiyo.

“Hadi sasa tumeshapata majina ya wachungaji watatu ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo viovu kwa wanafunzi
na uchunguzi bado unaendelea” alisema Bw. Kipozi.

Aliongeza kuwa, wachungaji hao wameanzisha mtandao wa kuwavizia wanafunzi wa kike katika vichaka vilivyopo kwenye
njia inayokwenda shuleni na kuwabaka.

Alisema hali hiyo imesababisha wanafunzi hao kuanza mgomo baridi wa kutokwenda shule wakipinga kufanyiwa vitendo hivyo. 

“Nimemwagaiza Mkuu wa Kituo cha Polisi Chalinze kuhakikisha mtandao huu unasakwa na kukamatwa, tukishindwa kuwapata tutawakamata waajiri na hatuta waachia hadi watuhumiwa watakapopatikana,” alisema.

Bw. Kipozi amewataka wazazi na wananchi kwa ujumla, kuwafichua watu wenye tabia ya kuwarubuni wanafunzi
wa kike ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment