02 April 2013

NCCR-Mageuzi waandamana kutaka amani


Na  Patrick Mabula, Kahama

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, kimewataka viongozi wa madhehebu ya dini nchini, vyama vya siasa na Serikali kutumia hekima na madaraka yao
vizuri ili kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kudumu.


Katibu Habari na Uenezi wa chama hicho Taifa, Kitengo cha
Vijana, Bw. Deogratias Kisandu, aliyasema hayo mjini Kahama
juzi katika mkutano wa hadhara uliokuwa na lengo la kuhubiri
amani, upendo na mshikamano kwa masilahi ya nchi.

Mkutano huo ulifanyika katika Viwanja vya CDT Mjini Kahama
na ulitanguliwa na maadamano ya kilomita mbili kutoka eneo la Phatomu Nyasubi hadi katika viwanja hivyo.

Bw. Kisandu alisema, lengo la matembezi hayo ni kusisitiza
amani ya nchi ambayo imeanza kuchezewa kwa misingi ya
udini na baadhi ya watu wenye malengo binafsi.

Alisema vipo baadhi ya vikundi ambavyo vimeanza kutumia
kivuli cha udini kutaka kuvuruga amani hivyo ni wajibu wa vyama
vya siasa, viongozi wa dini na Serikali kukemea hali hiyo.

Aliwataka vijana wakatae kutumiwa na wanasiasa kwa masilahi
yao bali wawajibike kulinda amani na utulivu uliopo ili kuepusha
machafuko yanayoweza kutokea na kusababisha maafa nchini.


Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama  ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Benson Mpesya, aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, hakuweza kufika baada ya kutoa udhuru.

No comments:

Post a Comment