02 April 2013

Wanafunzi 888 hawajaripoti shuleni



Na Suleiman Abeid,
Simiyu

ASILIMIA 48.4 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika shule za sekondari wilayani Meatu mkoani Simiyu hawajaripoti katika shule hizo hadi kufikia katikati ya mwezi Machi mwaka huu.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Ofisa elimu taaluma wa sekondari wilayani Meatu, Bi. Nchama Mchanga kati ya wanafunzi 1,718 waliokuwa wameteuliwa kujiunga na masomo ya sekondari ni wanafunzi 888 pekee ndiyo waliokwisha ripoti shuleni mpaka hivi sasa.

Bi. Mchanga alisema kati ya wanafunzi waliokwisha ripoti 519 ni wavulana na wasichana ni 369 sawa na asilimia 51.6 ya waliochaguliwa kujiunga na masomo hayo kwa mwaka 2013 katika shule zote za sekondari 22 zilizopo katika wilaya hiyo.

“Kwa kweli hali siyo ya kuridhisha, maana ni karibu nusu ya watoto wote waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari kwa mwaka huu hawajaripoti katika shule walizopangiwa, hatuelewi tatizo ni lipi, hata hivyo huenda wazazi wakawa ni
kikwazo kutokana na kutokuwa na mwamko wa elimu,” alieleza Bi. Mchanga.

Kutokana na hali hiyo baadhi ya wadau wa elimu wilayani humo waliokutana katika kikao cha kujadili changamoto mbalimbali zinazosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu walipendekeza kutungwa kwa sheria ndogo itakayowabana wazazi wanaozuia watoto
wao kwenda shule.

Pia wadau hao walipendekeza kuanzishwa kwa utaratibu utakaosaidia kuwaelimisha wazazi wilayani humo kuona umuhimu wa elimu kwa watoto wao na pawe panafanyika ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kudhibiti vitendo vya utoro mashuleni na
kuwachukulia hatua wanaume wanaobainika kuwapa mimba watoto wa shule.

Kwa upande mwingine mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Meatu, Bw. Isaya
Moses alisema katika kuboresha suala la elimu wilayani humo tayari halmashauri yake imetenga kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi walimu.

“Moja ya changamoto inayochangia matokeo mabaya ya elimu katika wilaya yetu, ni ukosefu wa nyumba za kuishi walimu, maeneo mengi walimu wanashindwa kuishi kutokana na kutokuwepo nyumba za kuishi, hali inayosababisha shule nyingi kuwa na uhaba
mkubwa wa walimu,”

“Tumepanga katika bajeti ya mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika maeneo ambayo yana mazingira magumu ya kufundishia, hata hivyo fedha hii tutaitoa kwa utaratibu wa kuishirikisha jamii, wao wakianzisha ujenzi wa boma sisi tunaezeka,” alisema Moses.




No comments:

Post a Comment