02 April 2013

Jk atoa zawadi ya pasaka kwa yatima DarNa Darlin Said

RAIS Jakaya Kikwete ametoa zawadi ya Sikukuu ya Pasaka yenye thamani ya zaidi ya shilingi mil.5 kwa vikundi tisa vya kulea watoto yatima na waishio katika mazingira magumu jijini Dar es Salaam.

Zawadi hizo alizikabidhi Kamishna wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Bw.Dunford Makala kwa niaba ya Rais Kikwete katika hafla fupi ya kukabidhi zawadi hizo iliyofanyika Dar es Salaam jana katika mahabusu ya watoto iliyopo Kisutu.

Bw.Makala alikabidhi mbuzi,mchele,na mafuta ambapo kila kikundi walipata vitu hivyo kwa viwango tofauti kulingana na idadi ya watu waishio katika vikundi hivyo, mbuzi wawili hadi watatu walitolewa,mchele kilo 100 hadi 150 na mafuta lita 10 hadi 40.

Alivitaja vikundi hivyo ni pamoja na Yatima Kurasini,Yatima group Chamazi,Chakuvama,Kwetu Mbagala Girls,Mahabusu ya watoto Upanga,Chuo cha ufundi cha wenye ulemavu,Makao Makuu Msimbazi center,Makao Makuu Nunge,pamoja na Makao ya wazee Msimbazi.

Akikabidhi zawadi hizo Bw.Mkala alisema rais Kikwete alitoa zawadi hizo kama ishara ya kuonyesha jinsi anavyo wathamini na kuwajali watu wa kundi hilo.

Hivyo amewataka wananchi wawe na moyo wa huruma na kuwajali pamoja na kuwatembelea kundi hilo ili na wapate faraja hasa katika siku hizi za sikukuu.

Mbali na vikundi hivyo rais Kikwete ametoa zawadi hizo kwa vituo vya mahabusu ya watoto vilivyopo Moshi,Arusha,pamoja na Mbeya.

Naye Mlezi wa Mahabusu ya Watoto Kisutu Bi.Magret Jackson akipokea zawadi hizo alisema wanafarijika kuona watoto walioishi hapo baada ya kutoka hapo tabia zao zinabadilika na kuwa watoto wenye nidhamu na kupenda kusoma.

"Kuna mtoto alikaa hapa kwa miezi sita baada ya kutoka hapo alijirebebisha kitabia na sasa ni mwanasheria aliyehitimu Chuo Kikuu cha Tumaini"alisema Bi.Magreti.

Kwa upande wa Muhudumu wa Kituo cha Watoto yatima Msimbazi center, Sister Maria Sirivana aliwaomba  wadau kuwa na moyo wa kuwaona watoto hao ili wajione nao wana wazazi wanaowajali .

Awali Mtoto anaeishi katika kituo cha Yombo Kiwalani Bw.Karuson Kigula baada ya kumshukuru raisi Kikwete kwa kuwakumbuka  alisema wanakabiliwa na upungufu wa walimu pamoja na kula chakula cha aina moja kwa muda mrefu.

"Mara nyingi tunakula Maharagwe na Ugali, wali ni mara moja kwa mwezi hivyo kupata msaada huo hasa katika kipindi hiki tumefurahi,"alisema Mtoto Kigula

  

No comments:

Post a Comment