02 April 2013

Walimu,wanafunzi waishi kinyumba

Na John Gagarini, Bagamoyo

MWALIMU wa Shule ya Msingi Msoga, iliyopo Wilaya ya Bagmoyo, mkoani Pwani, Bw. Joel Mjema, anatuhumiwa
kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo
(jina tunalihifadhi) hivyo kushindwa kuendelea na
masomo baada ya kumaliza darasa la saba.

Tuhuma hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha
pamoja kati ya wazee maarufu, viongozi wa dini, wajumbe wa Serikali ya Kijiji, Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Ahmed Kipozi.

Katika kikao hicho, mwalimu mwingine aliyefahamika kwa
jina la Bw. Samwel Mjema, naye alidaiwa kuishi kinyumba na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Msoga (jina tunalihifadhi).

Ilidaiwa kuwa, baada ya wazazi wa mwanfunzi huyo kubaini
mtoto wao anaishi kinyumba na mwalimu huyo, waliamua
kumalizana kimya kimya na mtuhumiwa.

Akizungumza katika kikao hicho juu ya tuhuma hizo, Bw.
Kipozi aliagiza walimu hao wasakwe na kukamatwa ili
wafikishwe mahakamani.

“Naambiwa mwalimu Joel Mjema pia aliwahi kumjaza mimba mwanafunzi mwingine aliyekuwa akisoma kidato cha tatu Shule
ya Sekondari Lugoba (jina tunalihifadhi), kumkatisha masomo
na kuishi naye kinyumba...hii ni aibu kubwa kwa mwalimu
ambaye amepewa dhamana ya kulea watoto kimaadili,” alisema.

Aliongeza kuwa, mwalimu Samwel Mjema alifumaniwa na wazazi wa mwanfunzi huyo lakini cha kushangaza suala hilo limemalizwa kimya kimya kati ya mwalimu huyo na wazizi husika.

“Kitendo hiki hakikubaliki, nataka huyu mwalimu akamatwe
na kuchukuliwa hatua mara moja pamoja na wazazi wa mwanafunzi kwa kufikia makubaliano ya kulimaliza suala hili jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi,” alisema Bw. Kipozi.

Alisema walimu hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikiuka maadili na kanuni za utumishi kwa kufanya ngono na wanafunzi
kitu ambacho sheria za nchi na taratibu za utumishi zinakataza.

Aliongeza kuwa, Serikali haiwezi kuvumilia uchagu huo hasa
kwa mtu anayepaswa kuheshimiwa kama mwalimu kuamua
kuwashawishi wanafunzi na kufanya nao ngono.

Bw. Kipozi alisema, jambo la kusikitisha zaidi ni wanafunzi hao kukatishwa masomo hivyo kukosa mwelekeo wa maisha ya baadaye.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema kuwa, mwalimu Swamel Mjema tayari amekamatwa kuhusiana na tuhuma hizo na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati mwalimu Joel Mjema, anadaiwa kutoroka na anaendelea kutafutwa.


No comments:

Post a Comment