02 April 2013

Walimu wadaiwa kuacha kukimbilia biashara zaidi
Na Timothy Itembe Tarime.

SERIKALI imetakiwa kukemea vitendo vinavyofanywa na baadhi ya walimu kutoa ajira juu ya ajira kwa kuwapa rushwa walimu wenzao ili kuwasaidia vipindi vyao darasani na wao kusafiri kwenda kufanya shughuli zao za kibiashara.


Hayo yalisemwa katika kikao cha wadau wa elimu ambacho kiliandaliwa na halmashauri ya wilaya Tarime mkoani Mara hivi karibuni,ambacho kiliandaliwa kwa lengo la kutadhimini changamoto  zinazowakabili Wanafunzi,Walimu pamoja na Wazazi.

Kikao hicho kilijumuisha kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya,Wadau mbalimbali wa elimu
pamoja na Maofisa Elimu Sekondari, Msingi Waratibu Elimu kata sanjari na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari.

Katika kikao hicho, Bi. Magreti Shirima alisema kuwa kushuka kwa elimu kumechangiwa na baadhi ya Walimu ambao sio waaminifu kazini ambao wameacha kazi waliyoajiriwa kwenda kufanya biashara zao na badala yake wanawatumia Walimu wenzao kuwasaidia kufundisha.

Bi. Magreti alisema kuwa walimu wengi wamejikita katika biashara zao binafsi badala ya kuzingatia kazi ya kufundisha ambayo ndiyo ambayo waliajiriwa na serikali kulitumikia Taifa kwa kufundisha watoto na kuwapa elimu ili kuondokana na ujinga.

Alisema kuwa hali kama hiyo inapotokea inachangia wanafunzi wengi kushindwa kujua kusoma na kuandika na kupelekea elimu kushuka hapa nchini.

Aidha imeelezwa kuwa hali kama hiyo inasabisha  walimu wengi kuwa watoro kazini bila kuchukuliwa hatua zozote, ambapo pia hali hiyo huchangia kushuka kwa elimu hapa wilayani Tarime na Tanzania kwa ujumla.

Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Mwita Waitara alisema kuwa kunahaja ya serikali,Halmashauri na viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa elimu kulitazama upya swala la elimu sanjari na kutazama upya athari zitakazotokea baada ya sekta ya
elimu kukabiliwa na changamoto lukuki.

Alisema katika kukalibiliana na changamoto hizo
kunahaja ya kutazama upana wa swala lenyewe ili kulitafutia uvumbuzi wa kudumu kwa muda muafaka ili kuokoa kizazi na Taifa kutokutumbukia gizani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Wilaya Tarime John Henjwele alisema kuwa atahakikisha anakabiliana na changamoto za elimu wilayani humo.

No comments:

Post a Comment