02 April 2013

Madereva pikipiki 85 wapatiwa semina elekezi



Na Abdallah Amiri,
Igunga.

JESHI la Polisi wilaya ya Igunga mkoani Tabora limewapatia semina elekezi madereva pikipiki na bajaji zaidi ya 85 juu ya taratibu na matumizi ya vyombo vya usafiri.

Akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika katika kituo cha polisi wilayani Igunga mhakiki wa vyombo vya usafiri kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA),Bw. Abduly Mohamed aliwataka madereva pikipiki na bajaji kufuata sheria na taratibu za matumizi ya vyombo vya usafiri.

Aidha, Bw. Mohamed aliwaeleza madereva hao kutambua kanuni za kujisajili zilizowekwa na Sumatra ili kupata leseni,Bima pamoja na leseni ya usafirishaji wa abiria ambayo hutolewa na ofisi ya Ofisa biashara wa halmashauri ya wilaya husika.

Katika semina hiyo, pia alitoa muongozo na masharti ya maombi ya leseni hizo na kusisitiza kuwa chombo chochote kinachosafirisha abiria lazima kiwe na ubao wa namba za usajili chenye rangi nyeupe ili kutambulika kuwa ni chombo kinachotumika kusafirisha abiria.

Naye Kaimu Ofisa Biashara wa Wilaya ya
Igunga, Bw.Thadeus Asely alifafanua maeneo yaliyotenga na halmashauri ya wilaya
hiyo kwa ajili ya maegesho ya pikipiki
na bajaji kuwa ni TTCL, Stendi mpya ya mabasi pamoja na eneo la hospitali ya wilaya hiyo.

Hata hivyo, Bw. Asely aliongeza kuwa,halmashauri ya wilaya hiyo imeweka mikakati ya kukarabati bna kuboresha vituo hivyo ili kuondoa usumbufu kwa madereva na abiria wanaotumia vyombo hivyo.

Nao madereva hao walilishukuru jeshi la
polisi wilayani hapa kwa kuwapa semina hiyo na kusema kuwa itawasaidia kujiepusha kutozwa faini zisizo za lazima na kuongeza kuwa kutokana na semina
waliyoipata juu ya utumiaji wa vyombo vya moto watahakikisha wanazingatia kwa makini ili kuepusha ajali za mara kwa mara .

Kwa upande wake Mkuu wa jeshi la polisi
wilaya ya Igunga Bw.Abeid Maige wakati akifunga semina hiyo amewataka madereva hao wazingatie semina waliyoipata na kuongeza kuwa wawe makini kutumia vyombo vya usafiri ili kuepusha ajali hasa katika msimu huu wa Sikukuu ya Pasaka.






No comments:

Post a Comment