02 April 2013

Wafukuaji vifusi Dar waokota vichwa *Waliokufa sasa wafikia 34, wahusika wote mbaroni


Na Goodluck Hongo

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Meck Sadiki, amesema idadi ya watu waliokufa katika tukio la kuanguka kwa ghorofa 16 katikati ya jiji hilo, imefikia 34 pamoja na vichwa viwili ambavyo vimefukuliwa kwenye kifusi lakini havina viwiliwili.

Akizungumza Dar es Salaama jana akiwa eneo la tukio ambalo waokoaji walihitimisha kazi hiyo, Bw. Sadiki alisema kazi ya
uokoaji na uondoaji kifusi ilichukua siku nne usiku na
mchana kuanzia Machi 29 mwaka huu.

Alisema Serikali itawachukulia hatua watu wote ambao itabainika walihusika na uzembe uliochangia jengo hilo kuporomoka.

“Leo (jana) natangaza rasmi kuwa kazi ya uokoaji na utoaji kifusi tumeimaliza, majeruhi waliobaki hospitalini hadi sasa ni wanne, wawili kati yao ni watoto wenye asili ya Kiasia,” alisema.

Aliongeza kuwa, miili iliyopatikana mwanamke ni mmoja pamoja
watoto ambao inadaiwa walikuwa wakicheza jirani na eneo la ujenzi na kuzishukuru kampuni mbalimbali zilizoshiriki katika uokoaji.

Alisema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kushirikiana na Serikali, watagharamia majeneza ya kuhifadhia miili ya watu waliopoteza maisha katika tukio hilo.

“Pia tutagharamia usafiri kutoka hospitali hadi katika nyumba ambazo watafanya ibada ya mazishi...miili ya watu ambao ndugu zao hawatajitokeza, Serikali itawajibika kuwazika lakini hadi sasa, maiti nyingi zimeshachukuliwa na ndugu zao.

“Tunamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kutembelea eneo la
tukio siku mbili pamoja na majeruhi waliolazwa Hospitalini ya
Taifa Muhimbili (MNH), Makamu wa Rais Dkt. Mohamed
Ghalib Bilal na Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, nao
walifika eneo la tukio nawashukuru,” alisema.

Alisema viongozi mbalimbali wa Serikali, Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange na Mkuu wa Jeshi la
Polisi IGP Said Mwema nao walifika kutokana na uzito
wa tukio lenyewe.

Bw. Sadiki alisema, Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imeunda tume ya uchunguzi yenye wajumbe watano wakiwemo Wahandisi
wawili kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wengine ni ofisa mmoja kutoka Jeshi la Polisi aliyebobea katika sheria na ofisakutoka TAMISEMI ambao watashirikiana na tume
ya Wahandisi iliyoundwa mwanzo kuchunguza tukio hilo.

Alisema taarifa za uchunguzi huo zitatolewa baada ya tume hiyo kutoa majibu yake na kama itathibitika jengo lililojengwa pembeni mwa hilo lililodondoka lipo chini ya kiwango, litabomolewa.

“Nawashauri wananchi waishio jirani na jengo ambalo linafanyiwa uchunguzi, wahame mara moja hadi ukamilike,” alisema Bw. Saidiki.

Dkt. Emmanuel Nchimbi

Akizungumza kwa niaba ya Rais Kikwete, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliwashukuru wananchi pamoja na vikosi vyote vilivyojitolea kufanikisha uokoaji.

“Rais amenituma nije kuwashukuru wananchi na vikosi vyote vilivyohusika na kazi ya uokoaji na Aprili 8 mwaka huu, rais atakutana na watu wote walioshiriki katika kazi hii Ikulu na
kula naye chakula cha mchana pamoja na wafiwa,” alisema.

Alisema Serikali inatoa pole kwa wananchi wote ambao kwa
namna moja au nyingine, wamefikwa na msiba huo mkubwa.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema watuhumiwa tisa wamekamatwa akiwemo Mchambuzi wa Ubora wa Majengo, Bw. Vedasto Ferdinand (39), mkazi wa Kimara, Dar es Salaam.

“Tukimaliza kuwahoji watu wote, jalada lao litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), ambaye baada ya kulisoma, ataandaa mashitaka ya watu wanaopaswa kufikishwa mahakamani.

“Natoa wito kwa Makandarasi na Wahandisi wetu, wafuate sheria na taratibu za ujenzi kwani kazi ya Jeshi la polisi ni kuwafanya watu watii sheria si kufanya uhalifu hivyo hatutasita kuwamakata wahusika wengine wote,” alisema Kamanda Kova.

Wakati huo huo, Mwandishi Suleiman Abeid kutoka Shinyanga anaripoti kuwa, Serikali imeshauriwa kuwachukulia hatua za kisheria watu wote ambao itabainika wamefanya uzembe ambao umesababisha kuporomoka kwa jengo hilo.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Askofu wa Kanisa la Tanzania Field Evangelism (TFE) mjini Shinyanga, Edison Mwombeki, katika Ibada ya Sikukuu ya Pasaka.

Alisema itashangaza kama Serikali itaendelea na utaratibu wa kuunda tume za kuchunguza matukio makubwa yanayotokea
nchini hata kama sababu za kutokea kwake zinaeleweka na
wahusika kufahamika lakini hawachukuliwe hatua zozote.

“Tukio la kuanguka kwa ghorofa 16 jijini Dar es Salaam
limenisikitisha sana, Watanzania wenzetu wasio na hatia
waliokuwa wakijitafutia riziki za kila siku wamepoteza
maisha, tumuombe Mungu azipumzishe roho zao, muda
tulionao si wa kuunda tume tuwajibishane.

“Wazembe wote lazima waadhibiwe, hatuwezi kuruhusu matukio haya yawe kama utamaduni wetu, maghorofa mengi yameporomoka na tume zinaundwa, zikimaliza kazi zinafungia ripoti kabatini bila kuna wahusika wakiwajibishwa, tunataka kuona hatua zikichukuliwa kwa wakati,” alisema.

Alisema kama Serikali itaendelea na utamduni wa kuunda tume, ataendesha ibada maalumu ya kumuomba Mungu achukue hatua kwa watu wote wanaoendelea kusababisha majanga kwa Taifa.

Katika hatua nyingine, Askofu Mwombeki amewaomba waumini
wa madhehebu mbalimbali nchini, kuliombea Taifa liwe na amani ambayo hivi sasa ipo hatarini kutoweka.

Alisema hali hiyo hivi sasa ipo katika hatari ya kutoweka iwapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa kwa kuhakikisha kila mtanzania anaulinda utulivu uliopo na kutoruhusu chokochoko za uchochezi wa aina yoyote ambazo zinaweza kusababisha amani
hiyo kutoweka na kwamba daima amani hailindwi na maandamano wala matumizi ya mabomu.

No comments:

Post a Comment