02 April 2013

Nimefuraishwa na mshi kamano wa CCM,Serikali'

'
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Taifa Abdallah Bulembo ameeleza kuridhishwa kwake na umoja, mshikamano uliopo baina ya CCM na serikali yake katika mikoa ya Shinyanga na Geita.


Bulembo alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki hii wakati akiagana na viongozi wa Chama na serikali baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani humo Shinyanga.

Alisema kwamba umoja na mshikamano huo ni kielelezo tosha cha kutekeleazwa kwa vitendo kwa Ilani ya Chama na hivyo kutaka udumishwe zaidi.

“Hivi ndivyo inavyotakiwa Chama na serikali muwe kitu kimoja. CCM ndiyo baba au mama na ninyi viongozi wenzangu mnatakiwa mjue kwamba mko hapo kwa ajili ya CCM.

“Nilivyokuwa mkoani Geita nilikuta umoja na mshikamano kama huu. Hivyo nawapongeza kwa hili na endeleeni kuwa kitu kimoja maana kidole kimoja hakiwezi kuvunja chawa,” alisisitiza Bulembo.

Alisema sehemu yoyote yenye mshikamano baina ya Chama na serikali, maendeleo hupatikana kwa haraka na njia ya wazi, lakini inapokuwa kinyume na hivyo hutokea migongano baina ya pande hizo mbili kila mmoja akijiiona yeye ndiyo zaidi hali inayochelewesha maendeleo ya wananchi.

“Nyie wenzetu mliopo serikalini ni watekelezaji wa Ilani yetu ya uchaguzi inatokana na Chama chetu. Ni vizuri mkalijua hilo ili kuondoa umimi,” alisema.

Hata hivyo, aliwataka viongozi hao kuisemea CCM kila wafanyavyo vikao na wananchi jinsi inavyotekeleza Ilani yake ya uchaguzi.

“Mnapoenda kufanya vikao vyenu msione aibu kukisemea Chama chenu maana wengine madamu wamekuwa watendaji wa serikali wanaogopa hata kusema “CCM oyee!” wakidhani kufanya hivyo ni kosa.

Bulembo alifafanua kuwa duniani hakuna serikali isiyoheshimu chama chake kilichoiweka madarakani kwakuwa ndicho chenye dhamana ya kuunda serikali.

“Mimi nashangaa sana. Wakati mwingine unaona viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa wilaya na mikoa wajiuliza maswali mengi bila kupata majibu pindi wanapotakiwa kuvaa sare za CCM.

“Sasa huko mitaani sawa, lakini hata mkihudhuria vikao vya Chama kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nako kuna dhambi kuzivaa?,” alihoji Bulembo na kufafanua kuwa kufanya hivyo si dhambi.

Bulembo alionya kuwa mwanachama au kiongozi yeyote atakayehudhuria vikao vyake vya Chama kama hatavaa sare za CCM atamtoa nje au kumsimamisha mbele ya wenzake ili apate aibu.

“Kama hamtaki kuvaa sare za CCM, basi pia msiingie kwenye vikao vya CCM vinavyowahusu kwa mujibu wa katika ya Chama. Sare za CCM ni utambulisho wa Chama chenu ndiyo maana kuna methali moja inasema kwamba ukipenda bonga, penda na ua lake,” alisema Bulembo.

Bulembo pia aliwageukia viongozi na wanachama wa CCM  kutoka katika ngazi mbalimbali na kuwataka wavae sare hizo pindi inapobidi ili wawe mfano kwa wengine.

Alisema mwanachama au kiongozi unapovaa sare za CCM, hakuna mtu atakayekuja kukuomba rushwa maana ataogopa kuwa unaweza kumfikisha katika vyombo vya dola.

Aliwaagiza viongozi hao kufanya mikutano ya hadhara ya wananchi mara kwa mara ili kuwaleza mafanikio yaliyoletwa na serikali ya CCM.

Bulembo alisema huo ni wajibu wa kila kiongozi kuwajibika katika sehemu yake ya kazi badala ya kushinda ofisini na kusubiri mshahara mwisho wa mwezi.








No comments:

Post a Comment