04 April 2013

UVCCM: hatupo tayari kuandamana



Na Heckton Chuwa, Moshi

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), mkoani Kilimanjaro, umesema hautashiriki wala kufanya maandamano yoyote yasiyo na tija badala yake wataweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo ya ukosefu wa ajira.

Mwenyekiti wa umoja huo mkoani humo, Bw. Frederick Mushi, aliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mawazo, Kata ya Soweto, Moshi Mjini, baada ya uzindua tawi jipya la vijana wa eneo hilo.

“Zipo changamoto nyingi ambazo zinawakabili vijana lakini kufanya mandamano si jawabu la kupata ufumbuzi wa changamoto husika badala yake unaweza kuongeza matatizo...jambo la msingi ni kujiunga pamoja na kuandaa mikakati,” alisema.

Alisema wapo baadhi ya wanasiasa ambao wanawashawishi vijana kufanya maandamano ili kutimiza malengo yao ya kisiasa lakini
wanapopata shinda, wanawaacha bila kuwapa msaada wowote.

“Umefika wakati wa vijana kujiepusha na wanasiasa wanaotaka kututumia kama daraja la kufanikisha malengo yao kisiasa badala yake tujiunge pamoja ili kukabiliana na changamoto zinazotukabili maana wanaoathrika zaidi na chanmgamoto hizi ni sisi,” alisema.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Moshi Mjini, Bw. Aggrey Marealle, aliwapongeza vijana hao kwa kuanzisha umoja huo na kuwataka wafikie ngazi ya juu zaidi
ili waweze kuanzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS).

Katika mkutano huo, Bw. Marealle aliwakilishwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoani humo, Bw. Shambe Sagaf, ambaye aliongeza kuwa, njia pekee ya vijana kupambana na
tatizo la ajira ni kujiunga na kuanzisha vikundi vya maendeleo
hivyo aliahidi kuwaunga mkono ili waweze kutimiza azma yao.

No comments:

Post a Comment