04 April 2013

Polisi wazima vurugu za CCM, CHADEMA



Na Bryceson Mathias, Mvomero

JESHI la Polisi Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, limefanikiwa kutuliza vurugu za uchaguzi wa kuwapata wajumbe
wa Mabaraza ya Katiba ngazi ya Wilaya, uliokuwa ukiratibiwa
na baadhi ya viongozi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.


Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike juzi katika eneo la Kichamgani Turiani ambapo vurugu hizo ziliibuka baada ya wananchi kumkataa
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Bw. Damson Minja asiongoze kikao kwa madai ya kushindwa kusoma mapato na matumizi tangu achaguliwe.

Diwani wa Kata ya Mhonda, Bw. Salum Mzugi na viongozi mbalimbali wa CCM, walishindwa kutuliza vurugu hizo na
kusababisha polisi kuingilia kati.

Kwa upande wake, Diwani wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bi. Julian Petro, aliwatupia lawama viongozi wa CCM na kudai ndio waliokuwa wakilazimisha kikao hicho kiongozwe na Bw. Minja.

Polisi wa Kituo cha Turiani, waliwataka viongozi wa vyama vyote watafute mwongozo na taratibu za sheria zinazopaswa kufuatwa ili kutatua mgogoro uliojitokeza.

Wananchi wa Kichangani Turiani wamekuwa na mgogoro na Bw. Minja kwa kipindi cha miaka mitatu wakidai kusomewa mapato
na matumizi ili waweze kuwa na imani naye.

No comments:

Post a Comment