04 April 2013

TUCTA waibana serikali kima cha mshahara


Na Gladness Theonest

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), kupitia Baraza Kuu la shirikisho hilo, limeitaka Serikali kuhakikisha ndani ya mwaka mmoja, wafanyakazi katika sekta zote wanalipwa kima cha mshahara kinachokidhi mahitaji yao na kama itashindwa, watashinikiza mgomo.

Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Bw. Nicolas Mgaya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio matano yaliyopitishwa na baraza hilo.

Alisema kikao cha baraza hilo kilichofanyika Machi 28 mwaka huu, kilibaini wastani wa kima cha mshahara wa sekta binafsi ni sh. 70,000 na sekta ya umma sh. 170,000.

“Viwango hivi havimuwezeshi mfanyakazi mwenye familia ya
watu wanne kuishi zaidi ya wiki moja, pia baraza limebaini kuwa, Serikali haioneshi dhamira ya kuboresha mishahara si kwamba haina uwezo bali ni kutokana na jeuri ya muda mrefu,” alisema.

Bw. Mgaya alisema, kutokana na hali hiyo wafanyakazi wengi wa ngazi zote wamejikuta wakiishi maisha magumu wakati Serikali ikiendelea kuingia mikataba mibovu isito na tija kwa Taifa.

“Tumetoa notisi ya mwaka mmoja kwa serikali kupandisha kima
cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, nasi tutafanya utafiti ambao utawezesha kujua kima gani kilipwe kama Serikali itashindwa, tutashinikiza mgomo,” alisema Bw. Mgaya.

Alisema miaka mitano iliyopita, wafanyakazi wamekuwa wakiilalamikia Serikali juu ya kodi kubwa inayokatwa katika
katika mishshara yao lakini wamekuwa wakipuuzwa.

Aliongeza kuwa, Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14, haitazingatia kilio cha wafanyakazi ili waweze kupunguziwa kodi hadi asilimia 11 na kama hali hiyo itatokea, watapinga uonevu huo.

“Baraza limebaini kuwa, katika malipo ya uzeeni kasi ya maboresho ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni ndogo...wafanyakazi wanaendelea kustaafu kwa malipo kidogo ya pensheni wakati mifuko husika ikiendelea kuneemeka,” alisema.

Bw. Mgaya alisema, baraza hilo limeazimia maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa mwaka huu, yafanyike mkoani Mbeya ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete na kauli mbiu itakuwa “Katiba Mpya izingatie usawa na haki kwa tabaka la wafanyakazi”.

1 comment:

  1. HAYA NI MANENO TU, MARA NGAPI MMESHINIKIZA SERIKALI NA HALI YA MFANYAKAZI IKO PALE PALE. NYIE KULENI MWONDOKE MUNGU ATALETA MANABII WATAKAOWAOKOA WAFANYAKAZI NA SIO NYINYI WALAFI TU. WAFANYAKAZI NI WATUMWA WA NCHI YAO HILO LINAELEWEKA.

    ReplyDelete