05 April 2013

Viongozi Fikisheni ushauri wa Dkt. Bilal kwa wananchi


MAKAMU wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal, juzi alifungua mkutano wa mwaka wa Utafiti ulioandaliwa na Taasisi ya Utafiti
wa Kuondoa Umaskini nchini (REPOA).

Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa,
ili Tanzania na jamii iweze kufikia maendeleo ya kweli, mabadiliko ya lazima lazima yawepo.

Alisema maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini, yatatokana
na jamii kubadilika kifikra na kila mmoja kuwajibika kwa yake
anayoyatenda si vinginevyo.

Dkt. Bilal alisema ni wajibu wa kila Mtanzania afanye kazi
kwa juhudi, maarifa, kujali uzalendo, kucha starehe, tamaa
na kujilimbikizia mali.

Sisi tunasema kuwa, hotuba ya Dkt. Bilal, ina maana kubwa kwa kizazi cha sasa kuona umuhimu wa kubadilika ili kujiwekea msingi mzuri wa maisha kwa kujituma na kufanya kazi kwa bidii.

Ushauri wa kiongozi huyo unatokana na ukweli kwamba, umasikini katika jamii kubwa ya Watanzania si msamiati mgeni tangu kipindi cha utawala wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Ili mtu apate mafanikio katika maisha yake au kutatua tatizo linalomsibu, kwanza lazima ajitambue hivyo kila anayeshiriki kutokomeza umaskini anapaswa kujua masikini ni nani?

Ipo dhana inayosema, mtu yeyote anayepata kipato chini ya dola moja kwa siku ni masikini. Baadhi ya wataalamu wa uchumi nao wanasema, mtu mwenye uhakika wa kujipatia mahitahi ya lazima kama chakula, malazi na mavazi si masikini.

Katika upande wa chakula, huangaliwa uwezo wa mtu kumudu milo mitatu kwa siku. Katika malazi huangaliwa nyumba anayoishi na familia yake na jinsi awavyoweza kumudu mahitaji ya siku.

Wapo wanaosema Tanzania ni miongoni mwa nchi masikini
ambayo hupimwa kutokana na uchache wa pato la Taifa kwa mwaka, matumizi ya duni ya teknolojia, ukosefu wa huduma
muhimu kwa baadhi ya wananchi, miundombinu hafifu,
madeni, upatikanaji wa maji safi, salama na uwezo mdogo
wa kuzalisha katika sekta ya kilimo na viwanda.

Kutokana na vipimo hivyo, kundi hilo linaamini Taifa na watu
wake ni masikini kwa sababu fikra zao zinawatuma hivyo.

Imani yetu ni kwamba, sababu kubwa inayochangia Watanzania wengi kukata tamaa ya maisha ni umasikini wa fikra unaowafanya waogope kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo.

Kwa mfano, mtu ana shamba kubwa lenye miti badala ya kutafuta wataalamu ili afuge nyuki na kuzalisha asali, anaona bora anunue shoka ili akate magogo na kuchoma mkaa au kuuza mbao.

Dhana ya umasikini husababisha baadhi ya wananchi kutotambua mustakabali wa maisha yao hivyo vita wanavyopigana kupambana na umasikini huifanya kwa mazoea.

No comments:

Post a Comment