05 April 2013

M/kiti CCM kizimbani Dar kwa kujipatia milioni 500/-



Na Rehema Mohamed

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, Bw. Ayub Chamshama (68), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kujipatia fedha sh. milioni 500 kwa njia ya udanganyifu.

Mstakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Bw. Said Chamshama (31), ambaye ni mfanyabiashara mkazi wa Tegeta Nyaishozi.

Mbele ya Hakimu Geni Dudu, wakili wa Serikali Charles Anindo, alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo mwaka 2007 kwenye tarehe tofauti.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa watuhumiwa hao katika
tarehe tofauti walikula njama ya kutenda kosa. Shtaka la pili linamkabili Bw. Ayub pekee ambaye inadaiwa Oktoba 16,2007,
jijini Dar es Salaam, alighushi hati ya dhamana ya nyumba ya famailia kiwanja namba 12 Jangwani, yenye hati namba 28181 kuonesha kwamba ni yake.

Shitaka la tatu, washtakiwa wote katika tarehe isiyofahamika jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya waliwasilisha hati hiyo ya kughushi yenye jina la Abdi Ally Salehe katika Benki ya Kenya (KCB) kwa ajili ya kujipatia mkopo.

Watuhumiwa hao pia walisomewa shtaka la kujipatia fedha kwa
njia ya udanganyifu, ambapo walidaiwa tarehe isiyofahamika Dar es Salaam, katika beki ya KCB tawi la Samora, kwa njia isiyo halali walijipatia mkopo wa sh. milioni 500 baada ya kuwasilisha hati
ya kughushi.

Hata hivyo, washitakiwa hao walikana mashitaka hayo ambapo Wakili Anindo alidai upelelezi haujakamilika na kuomba
tarehe ya nyingine ya kutajwa.

Hakimu Dudu aliahirisha shauri hilo hadi leo kwa ajili ya kutoa masharti ya dhamana na kusema washitakiwa watarudi rumande.
 

1 comment:

  1. Mimi nadhani ni upuuzi watu kutumia muda mwiiingi kujadili eti nani achinje. Kwani Mkristo akila nyama iliyo chinjwa na waislamu atakufa? Au Muislamu akila iliyo chinjwa na Mkristo atakufa?

    Mimi ni Mwislamu lakini imani ni kwa Allah na sio kwenye vyakula, hizi ni mbinu zilizowekwa ili kuwapa waislamu mamlaka ya kuchinja tu kwani hata kitabu chetu kinasema kama mnyama amechinjwa na asiyekuwa muislamu basi tuombe dua kabla ya kula.

    Nyama yoyote iliyochinjwa mimi nakula bila kujali kachinja muislamu, mkristo au mpagani isipokuwa nguruwe.

    Leo tujihadhari kwani imani ni rohoni na si kwenye vitu tunavyoyumia.

    ReplyDelete