02 April 2013

Malecela awarushia kombora CHADEMANa Mwandishi wetu,Singida

MJUMBE wa Baraza Kuu la Jumuia ya Wazazi Taifa, William Malecela amekionya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuwa kisitegemee ushindi wa “chee” katika uchaguzi mkuu ujao.


Malecela alisema kuwa katika uchaguzi huo, CHADEMA  kitarajie kupata kura za huruma kutoka kwa wananchi tofauti na ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliyopita ambapo walipata idadi kubwa ya wabunge na madiwani.

Alitoa onyo hilo juzi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliyofanyika katika kituo cha zamani cha mabasi yaendayo mikoani mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Malecela, ushindi huo wa CHADEMA walioupata katika uchaguzi mkuu uliyopita ulitokana na mifarakano ya wana-CCM na hivyo kuamua kukisaliti chama chao na kukipigia kura chama hicho.

“Leo nawakumbusha kwamba ushindi wenu haukutokana na wafuasi wenu, bali wa CCM baada ya kufarakana wakati wa kura za maoni.

“Kutokana na mifarakano hiyo ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya CCM, ndipo baadhi waliasi na kuwaunga mkono kwa kuwapigia kura vingnevyo mngekula jeuri yenu kwa kuambulia patupu,” alisema Malecela.

Alisema kwa sasa CCM imejifunza mengi kutokana na mifarakano hiyo na imekuwa ikifanya vikao vya mara kwa mara nchi nzima ili kuondoa tofauti zilizojitokeza wakati huo na kufungua ukurasa mpya kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao.

“Sisi tumekuwa tukifanya vikao kwa ajili ya kumaliza tofauti zetu na baada ya vikao hivyo, sasa tumeungana pamoja na kuja kwenu wananchi wetu kufanya mikutano ya hadhara tukiwa kitu kimoja na ndiyo maana leo mnaona wote tuko hapa,” alisema.

Kwa upande wake mjumbe wa Baraza Kuu la umoja huo Taifa, Dk. Damas Mugasa, aliwataka wananchi waendelee kuiamini CCM na serikali yake kwa kuipa kura kwa sababu ndiyo chama pekee chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo.

Alisema CCM ni chama makini na sikivu, hivyo kina kila sababu ya kuchaguliwa ili kiweze kuleta maendeleo ya uhakika kwa wananchi wake.

“Hivi vyama vya upinzani havina tofauti na shetani. Hivi ni vyama vya mpito visivyokuwa na uwezo wa kuwaletea maendeleo…msihangaike navyo maana havina muelekeo,” alisema Dk. Mugasa.

Hata hivyo, Mugasa alisema kuwa katika uchaguzi mkuu ujao CCM imejipanga kimamilifu kukabiliana na wapinzani kwa kujivunia Ilani yake ya Uchaguzi.

Alifafanua kuwa kambi ya upinzani haina mvuto kwa wananchi kutokana na sera zao kutokidhi matakwa ya wananchi wenye dhamana ya kuwachagua.


No comments:

Post a Comment