02 April 2013

Serikali imeombwa kuwanusuru Wabarabaig

Na Martha Fataely,Moshi.

SERIKALI imeombwa kutafakari vyema mpango wake wa kuwahamisha wafugaji
wa asili ya Kibarabaig wanaoishi msitu wa pongwe wilayani Pangani
mkoani Tanga kwa kuwatengea maeneo maalum ya kuishi kabla ya kuwaondoa
maeneo hayo.


Rai hiyo imetolewa na asasi 20 zinazojihusisha na utetezi wa haki za
jamii ya wafugaji asili  nchini (TPCF) katika mkutano wao unaofanyika
mjini moshi  ambao ulijadili kwa kina suala la kuhamishwa kwa wafugaji
hao.

Asasi hizo zimeeleza kutopendezwa na hatua ya serikali wilaya hiyo
kuwafukuza wafugaji hao kwa kuwavunjia nyumba, kuharibiwa mazao na
biashara zao kwa madai kuwa ni  wahamiaji haramu.

Akizungumzia suala hilo,mratibu wa asasi kutoka mikoa yote nchini,ndg
joseph panasambei amesema, hatua ya serikali imeathiri zaidi ya
wafugaji 400 ambao wameishi katika msitu huo kwa zaidi ya miaka 12.

Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mkutano huo wamependekeza
serikali ichukue hatua za maksudi kuwahamisha mapema wafugaji au
wakulima wanaovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za taifa
au hifadhi za barabara kabla hawajajenga majengo ya kudumu.

Wamesema pamoja na kutengwa kwa maeneo maalum ya kisheria kwa ajili ya
wafugaji, wakulima na hifadhi za misitu za taifa ni vyema wahamiaji
wakapewa tahadhari na kuondolewa kabla hawajaweka makazi ambayo
baadaye yataleta migogoro isiyo ya lazima.

Walisema wafugaji hao sasa wanahangaika ndani ya nchi yao kama
wakimbizi bila kujua watalala na watakula wapi na kuiomba pia serikali
iwapatie misaada ya kibinaadamu kama chakula na malazi ya muda.

No comments:

Post a Comment