02 April 2013

Jukwaa la afya EAC lazinduliwa mjini Kigali



Na James Gashumba, EANA

JUKWAA la Afya Afrika Mashariki (EAHP), limezinduliwa juzi mjini Kigali, nchini Rwanda ambapo Serikali za nchi wanachama, zimetakiwa kushirikiana na jukwaa hilo kwa manufaa ya jamii.

AEPA ni taasisi inayolenga kuwezesha, kuboresha sekta ya afya
na kuleta maendeleo katika taasisi za afya, kuoanisha sera na sheria za sekta ya afya katika kanda ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA), jukumu la taasisi hiyo pia ni kutoa msukumo kwa sekta binafsi na asasi za kiraia juu ya masuala ya afya na wataalamu kutoka nchi wananchama wa EAC.

Akizindua taasisi hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa EAC ambaye anashughulikia Tija na Sekta ya Jamii, Jessica Eriyo, alisema
juhudi hizo zitasaidia kuboresha sekta ya afya katika kanda.

“Tunahitaji watu wenye afya na wazalishaji ambao wananufaika na ubora, unafuu wa huduma za afya katika kanda...hii si kwamba inaendana na mkakati wa mkakati wa EAC bali ni pamoja na
mikakati ya sasa ya maendeleo Afrika Mashariki,” alisema.

Alisisitiza kuwa ni muhimu Serikali za nchi wanachama kushirikiana na sekta binafsi ili kuunga mkono juhudi za kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Eriyo alitoa wito wa kuwepo kwa kampeni zaidi ili kuelimisha wananchi juu ya masuala ya afya katika ngazi za chini ambako asilimia 70 ya magonjwa yanayosumbua wananchi yanaweza
kuzuilika.

Mwenyekiti wa EAHP, Dkt. Amit Thakker, alisema watu wengi bado wanaugua magonjwa yanayoweza kuzuilika.

“Tumezindua jukwaa hili ili tuone kitakachofuata katika kushughulikia changamaoto zinazoikabili sekta hii kwa kupeana taarifa na kufanyakazi pamoja,” alisema Thakker.

No comments:

Post a Comment