02 April 2013

Darala Mto Kirurumu lakatika, abiria wakwama



Na Sophia Fundi, Karatu

IDADI kubwa ya abiria waliokuwa wakitokea Serengeti na Ngorongoro wengi wao wakiwa watalii, jana walishindwa
kuendelea na safari baada ya Daraja la Mto Kirurumu kukatika.

Daraja hilo linalounganisha Wilaya ya Karatu na Monduli,
mkoani Arusha ambapo hali hiyo ilisababishwa na mvua
kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana.

Mwandishi wetu alifika eneo la tukio na kukuta abiria hao wakihangaika kutaka kuvuka upande wa pili ili kuendelea na
safari zao lakini walishindwa kuvuka kutokana na wingi wa
maji na mawe makubwa yaliyosomwa na kujaa barabarani.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Bw. Felix Ntibenda, alifika eneo hilo na kuwataka abiria hao kuwa na subira
wakati Serikali ikiangalia uwezekano wa kurudisha mawasiliano.

Bw. Ntbenda alitoa agizo kwa polisi walioko Kituo cha Manyara, kuzuia magari yote yanayotokea Karatu ili kupunguza msongamano katika eneo hilo.

Daraja hilo linakatika kwa maara ya pili ambapo mwaka 2011, lilikatika na kusababisha abiria waliokuwa wakisafiri kwenda
maeneo mbalimbali, kukatisha safari zao ambapo Serikali
ilitumia wanajeshi kutengeneza daraja hilo.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya abiria waliokuwa wakitoka Karatu kwenda Dar es Salaam, waliitupia lawama Serikali kwa madai ya kushindwa kujenga daraja la kudumu.

No comments:

Post a Comment