02 April 2013

Mhasibu OUT kortini kwa kutakatisha mil. 578/-


Na Rehema Mohamed

MHASIBU wa Chuo Kikuu Huria nchini (OUT), Bw. Engels Mrikaria (42), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kutakatisha fedha zaidi ya sh. milioni 578.

Mshtakiwa alisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Agness Mchome na mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Katibu Muhtasi wa Chuo cha Biashara (CBE), Bi. Rose Maungu (45).

Wakili wa Serikali, Bw. Teophil Mutakyawa, alidai mahakamani hapo kuwa, mshtakiwa Bw. Mrikaria anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai 2009 hadi Aprili 2011.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa mshtakiwa huyo alifoji hati
za malipo ili kuonesha kuwa, Bi. Maugu, Bw. Boniface Msofe,
S.M January, W.F Charles, H.Kiungu na M.Mohamed ni waajiriwa wa Chuo Kikuu Huria nchini hivyo wanastahili kulipwa mishahara ya mwezi sh. 578,501,000.

Shtaka la pili ilidaiwa katika tarehe tofauti kati ya Julai 2009 na Aprili 2011, jijiji Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alijipatia kiasi hicho cha fedha kutoka akaunti namba 01113002560 NBC, Tawi
la Corporate la Chuo Kikuu Huria nchini.

Ilidaiwa mshrakiwa huyo alidanganya kuwa, fedha hizo zilikuwa mishahara ya kila mwezi kwa watu hao kitu ambacho hakikuwa
cha kweli.

Mshtakiwa huyo pia anadaiwa katika tarehe hizo Dar es Salaam
kwa nia ovu, alihamisha kiasi hicho cha fedha kutoka akaunti ya chuo hicho kwenda akanti za watu mbalimbali ikiwemo ya Bi. Maugu wakati akijua fedha hizo zilipatikana kwa kugushi.

Shtaka la nne linamkabili Bi. Maugu ambaye inadaiwa kuwa, kati
ya Aprili 2010 na Mei 2011, Dar es Salaam, alitakatisha sh. milioni 68 kutoka akaunti 011103002560 ya Chuo Kikuu Huria kutoka Benki ya NBC, Tawi la Corporate wakati akijua fedha hizo zilipatikana kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa wote, walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashtaka ulidai kuwa, upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Mchome, aliieleza mahakama hiyo kuwa maelezo ya
awali yasomwe Aprili 4 mwaka huu, ambapo washtakiwa wote wamerudishwa rumande.



No comments:

Post a Comment