26 March 2013
WAMA yapongezwa kwa kusaidia wanawake
Na Anna Nkinda, Maelezo
MKE wa Rais wa China Mama Peng Liyuan, amezipongeza kazi zinazofanywa na Mke wa Rais Tanzania, Mama Salma Kikwete kupitia taasisi anayoiongoza ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).
Alisema taasisi hiyo inawainua wanawake kiuchumi na kuwasaidia
watoto wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi kupata elimu sawa na watoto wengine.
Pongezi hizo zimetolewa Dar es Salaam wakati Mama Liyuan alipotembelea Ofisi ya WAMA ili kuona kazi wanazozifanya na kutoa zawadi ya vyerehani 20 vya kudarizi kwa ajili ya Umoja
wa Vikundi vya WAMA (UVIMA) na mabegi ya shule 100
kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya Sekondari WAMA-Nakayama, iliyopo Nyamisati, Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani.
Mama Liyuan alisema kuwa kupitia taarifa mbalimbali alizozisoma
ameweza kufahamu kazi na juhudi za Mama Kikwete anazozifanya za kuisaidia jamii na ataangalia jinsi gani anawezea kumuunga mkono kutokana na kazi anazozifanya.
Kwa upande wake, Mama Kikwete alimpongeza Mama Liyuan
kwa kuitembelea Tanzania muda mfupi baada ya mume wake
kuwa madarakani ambapo kitendo hicho kinaendeleza ushirikiano
na urafiki uliopo kati ya Tanzania na China.
“Naomba tuendelee kushirikiana katika kutatua matatizo ambayo yanawakabili wanawake na watoto wa kike kwani changamoto zao zinafanana duniani kote hivyo ni muhimu kuzifanyia kazi,” alisema.
Naye Bi. Tatu Ngao ambaye ni Mwenyekiti wa UVIMA, alimshukuru Mama Liyuan kwa kuwapa msaada wa vyerehani ambavyo vitawasidia kuongeza ujuzi na kuinua kipato chao
hivyo kujikwamua kiuchumi.
Alisema ndani ya UVIMA kuna vikundi vya 35 vya maendeleo ambavyo ni mchangiko wa wanaume na wanawake ila asilimia kubwa ya wanachama ni wanawake kutoka Kata ya Majohe
Gongolamboto, Dar es Salaam.
“Jambo la muhimu ni wanawake kujiunga katika vikundi vya maendeleo na kuhakikisha vimesajiliwa ili waweze kufikika
kirahisi na kujikwamua kiuchumi,” alisema Bi. Ngao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bi. Winfrida Leonard
ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama, alisema zawadi ya mabegi waliyopewa itawasaidia
kutunzia madaftari na vifaa vingine.
“Niishukuru WAMA kwa kutusaidia kielimu kwani tunasoma
bure bila ya kuchangia kiasi chochote cha fedha na tunapata
mahitaji yote muhimu kama chakula, maladhi na mavazi,” alisema.
Aliiomba Serikali iwawasidie watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi ambao wamekosa nafasi ya kusoma kwa kuwakusanya pamoja na kuwapa elimu kama alivyofanya Mama Kikwete kwani watoto ni Taifa la kesho.
Mama Peng Liyuan aliambatana na mkewe kwa ziara ya siku mbili nchini ambayo imeisha jana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment