13 March 2013

Wawakilishi Z'bar wamuomba IGP Mwema kuboresha makazi ya askari




Na Mwandishi Wetu

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, jana amefanya mazungumzo na wajumbe tisa wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi kutoka Zanzibar chini ya Mwenyeketi wake Bw. Hamza Hassan Juma.


Mazungumzo hayo yalifanyika Makao Makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam, ambapo Bw. Juma, alilipongeza Jeshi la Polisi nchini jinsi lilivyotekeleza maboresho yake licha ya changamoto nyingi zinazolikabili.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Msemaji wa jeshi hilo nchini, ASP Advera Senso, alisema katika kikao hicho, wajumbe hao walimuomba IGP Mwema, kuendelea kuboresha makazi ya askari Polisi yaliyopo Zanzibar ili waweze kuishi katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kufanya kazi zao bila bughudha.

Alisema wajumbe hao pia walitoa mapendekezo ya kuendelea kuboresha masilahi ya watendaji wa jeshi hilo ili yaweze kuendana na hali halisi ya maisha kwa sasa kwani kazi wanayoifanya ni kubwa
inayopaswa kuungwa mkono.

Aliongeza kuwa, pendekezo jingine ni elimu ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi iendelee kutolewa Zanzibar ili wananchi wengi waweze kuifahamu na kuitekeleza kwa vitendo ili kudumisha
amani na utulivu visiwani humo.

“Pia wajumbe hawa wameliomba Jeshi la Polisi lisisite kuchukua hatua wala kuwaonea huruma watu wote wanaochochea vurugu,”
alisema ASP Senso.

Alisema katika kikao hicho, IGP Mwema na wajumbe hao kwa pamoja waliazimia kukutana mara mbili kwa mwaka upande wa Zanzibar na mara moja Tanzania bara.

“Lengo ni kuweka mikakati ya kuimarisha usalama nchini pamoja
na kufanya semina za mara kwa mara ili kujifunza dhana nzima ya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii,” alisema.

IGP Mwema aliahidi kuboresha makazi ya mbwa na farasi upande wa Zanzibar na mikoa mingine ya Tanzania ili kuimarisha ulinzi na usalama kwa kutumia vitendea kazi hivyo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Alli Mussa, amesema wataendelea kuboresha makazi ya askari kwa kutumia rasilimali zilizopo na kuwashirikisha wadau wa ndani na nje.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Kamishna wa Polisi Utawala
na Rasilimali, CP Clodwig Mtweve, Kaimu Katibu Mkuu Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Agustino Shio, Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano, Lupi Mwaikambo na Maofisa Wakuu Waandamizi wa jeshi hilo Makao Makuu.

No comments:

Post a Comment