13 March 2013

Mwenyekiti CHADEMA asimamishwa uongoziNa Wilhelm Mulinda, Mwanza

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kata ya Ilemela, mkoani Mwanza, kimemsimamisha uongozi aliyekuwa Mwenyekiti wa kata kwa tiketi ya chama hicho, Bw. Isack
Nyatega, kutokana na tuhuma mbalimbali.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Kata wa CHADEMA, katika kata hiyo, Bw. Sosthenes Salvatory, alisema uamuzi huo ulifikiwa kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho wa kata,
ambao ulifanyika hivi karibuni.

Alisema Bw. Nyatega, anatuhumiwa kutumia madaraka yake
vibaya kinyume cha katiba ya chama hicho kwa kujichukulia
uamuzi wa kufuta matawi ya wanachama.

Tuhuma nyingine ni kuvuruga mikutano ya hadhara ya Umoja wa
Vijana wa Chama hicho (BAVICHA), kwa kuwatishia kuwaitia polisi ili wakamatwe kama wataendelea kuifanya.

Bw. Salvatory aliongeza kuwa, tuhuma nyingine ni kung’ang’ania vifaa na nyaraka za chama kama mihuri, maazimio ya vikao pamoja
na daftari la wanachama.

“Pia Bw. Nyatega anatuhumiwa kutaka kumnyang’anya kadi ya uanachama Diwani wa kata hiyo, Bi. Marietha Chenyenge, wakati kamati tendaji ya kata ndio yenye jukumu la kufanya hivyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, kutokana na tuhuma hizo Mkutano Mkuu wa kata umemteua Bw. Michael Sayayi, kuwa Mwenyekiti wa muda hadi utakapofanyika Uchaguzi Mkuu Mei mwaka huu.

No comments:

Post a Comment