04 March 2013

Wauza samaki Feli wafungiwa geti na uongozi




Na Anneth Kagenda

MAGARI yaliyobeba samaki, jana yalifunga babaraba katika Soko
la Kimataifa la Feli baada ya uongozi wa soko hilo, kufunga geti ambalo hutumiwa na magari hayo kuingiza samaki sokoni hapo.

Hali hiyo ilisababisha foleni kubwa katika barabara hiyo ambapo wafanyabiashara waliopeleka samaki sokoni hapo kwa kutumia magari hayo, walikuwa wakiushinikiza uongozi wa soko hilo ufungue mageti ili waweze kuingiza samaki wao.

Tukio hilo limetokea jana ambapo baadhi ya wafanyabiashara
hao walisikika wakisema, samaki waliopakiwa kwenye magari
yaliyozuiwa kuingia sokoni hapo wana thamani ya zaidi ya
sh. milioni 60 hadi 70.

Wakizungumza na Majira sokoni hapo, wafanyabiashara hao walisema magari hayo yaeandelea kuziba barabara hadi kilio
chao kitakaposikilizwa na Serikali.

“Kimsingi Serikali inatunyanyasa sana, mambo tunayofanyiwa
sisi wafanyabiashara wa samaki sokoni hapa si ya kiungwana
hivyo tumechoka kunyanyaswa,” alisema Bw. Jumanne Shaweji
ambaye ni Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wakusanyaji
Samaki na Wauzaji (UWASAU) zoni namba nane 'B'.

“Eneo hili linataka kumilikishwa kwa watu wengine badala ya
kutupa sisi wazawa, awali tuliwaona raia wenye asili ya Asia
wakilipima na wafanyabiashara wakubwa ambao tumewahi kuwaona katika kampuni mbalimbali.

“Uongozi wa soko ulitupa siku saba tuache kushusha samaki eneo hili ambazo zinakwisha Machi 7 mwaka huu, lakini leo (jana), tunashangaa kuona kabla siku hazijaisha geti limefungwa na sisi kuambiwa haturuhusiwi kuingiza samaki,” alisema Bw. Shaweji.

Aliongeza kuwa, wamewahi kufanya mawasiliano na uongozi
wa soko ili wakae pamoja ili kama tatizo ni ushuru kuwa mdogo kama walivyowahi kuambiwa wajue nini cha kufanya lakini hadi
jana jambo hilo lilikuwa halijapatiwa ufumbuzi wowote.

“Samaki wetu wanaendelea kukaa kwenye magari kama
unavyoona na mengi hayana barafu hivyo uwezekano wa
kugaribika ni mkubwa na sisi kupata hasara,” alisema.

Bw. Saidi Bakali alisema, manyanyaso dhidi yao ni mengi na hawathaminiwi mbali ya kwamba wao ndio wadau wakubwa
wa biashara hiyo lakini bado wanakandamizwa.

Awali wafanyabiashara hao walidai hawawezi kuondoka eneo hilo hadi Serikali iwatafutie eneo lingine wakiamini eneo hilo linataka kutolewa kwa wafanyabiashara wabungwa.

No comments:

Post a Comment