04 March 2013

Makamba: Nachonganishwa na CCM


Na Yusuph Mussa, Korogwe

KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Yusuf Makamba, amesema baadhi ya vyombo vya habari nchini vinamchonganisha na chama chake.

Alisema pamoja na kustaafu nafasi hiyo, hawezi kusimama katika majukwaa na kukisema chama chake vibaya kwani kabla hajawa Katibu Mkuu, alipitia ngazi nyingine kama Katibu wa Tawi.

Mzee Makamba aliyasema jana wakati anazungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake mjini Korogwe, mkoani Tanga wakati akikanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti moja (si Majira).

Alisema katika gazeti hilo ukurasa wa mbele, lilikuwa na kichwa
cha habari kinachosema “Mzee Makamba anena: Mungu ataiadhibu CCM” na kudai habari hiyo imepotosha ukweli wa alichozungumza kwenye uzinduzi wa Halmashauri Mpya ya Bumbuli, wilayani Lushoto Februari 23 mwaka huu.

“Mimi sikusema Mungu ataiadhibu CCM, rasilimali yangu ni jina langu, mwandishi alitaka kuchafua jina langu wakati mimi ni mtiifu kwa chama changu na viongozi wake.

“Nimeitumikia CCM tangu nikiwa Katibu wa Tawi, naomba waniombe radhi...mimi sina njaa, nimelipwa kiinua mgongo
kizuri baada ya kulitumkia Taifa kama Mkuu wa Wilaya,
Mkuu wa Mkoa na Mbunge,” alisema.

Bw. Makamba alisema, katika habari hiyo mwandishi alidai yeye ndiye aliyesababisha CCM kukosa mvuto mbele ya jamii jambo ambalo halina ukweli kwani ndani ya uongozi wake 2006-2011, chama hicho wabunge wengi walitoka chama tawala.

“Kusema chama kimekosa mvuto kwa ajili yangu ni upuuzi,
nikiwa Katibu Mkuu, Rais alishinda kwa asilimia 61, huu ni
ushindi mkubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, alichosema katika hotuba yake ni kuhamasisha wananchi waendelee kuchangia nguvu zao kwenye miradi yote
ya maendeleo kwani fedha zinazopelekwa katika halmashauri
ni kidogo na viongozi wa halmashauri wawe makini nazo.

“Pia niliwataka watumishi wa halmashauri wawe waadilifu kwa fedha kidogo zinazotengwa zisiingia mifukoni mwao, niliwataka wajiepushe na rushwa...kwa mujibu wa Biblia na Quran, rushwa
ni dhambi.

“Nilinukuu mistari ya Quran inayosema, msiliane mali zenu kwa batili mkazi peleka kwa mahakimu wakati mkijua kufanya hivyo
ni dhambi, kitabu cha Biblia kinasema, msipokee rushwa, maana hupofusha macho hao waonao,” alisema Bw. Makamba.

No comments:

Post a Comment