11 March 2013

'Waumini Anglikana tumuombee Dkt. Mokiwa'



Na Anneth Kagenda

WAUMINI wa Kanisa la Anglikana nchini, wameshauriwa kuzama katika maombi na kuiombea familia ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dkt. Valentino Mokiwa, ambaye mwishoni mwa wiki alivamiwa nyumbani kwake Mbezi Luis, Dar es Salaam,
eneo la Mashirikiano na watu wasiofahamika.

Watu hao baada ya kumkosa Askofu Mokiwa, walimjeruhi mlinzi
wake Bw. Fred Fute (29), mkazi wa Mbezi, ambaye alicharangwa mapanga ambapo taarifa zaidi zinasema, mlinzi huyo amelazwa katika Hospitali ya Tumbi, mjini Kihaba, mkoani Pwani kwa matibabu zaidi.

Baada ya kumalizika kwa ibada iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, mtoa matangazo aliwashauri waumini wa kanisa hilo kuzama kwenye maombi, kuiombea familia ya Askofu Mokiwa, ili kumnusuru na majanga mbalimbali.

“Ni vyema kila mtu kwa nafasi yake akafanya maombi kwa
ajili ya familia ya Askofu wetu wakati Jeshi la Polisi nchini likiendelea kufanya upepelezi wa tukio hili,” alisema mtoa
matangazo kanisani hapo.

Awali akitoa mahubili, Padri John Magafu, aliwataka waumini wa kanisa hilo kipindi hiki cha kwaresma ni muhimu kwa kila mmoja kuzama kwenye maombi.


“Tunatakiwa kuishi kwa neema ya Mungu kwani hakuna aliye mkamilifu mbele za Bwana hivyo tunapaswa kuomba hasa
kipindi hiki cha kwaresma ambacho kanisa linajaribiwa na kutikiswa,” alisema Padri Magafu.

Alisema lengo la kusisitiza maombi kwa waumini ni kutokana na vitendo mbalimbali vinavyojitokeza nchini hivyo ni wakati wa kutubu, kufunga na kuomba ili kujisafisha mbele za Mungu.

Hata hivyo, aliwataka waumini kutoligeuza kanisa kama kijiwe na kuacha manung'uniko kwani kukaa na hali hiyo ni moja ya sababu inayoweza kuwafanya wasifike mbinguni.

“Hivi sasa nchi yetu inalalamikia umaskini uliopo, wananchi wana kero nyingi ikiwemo ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, lakini ikumbukwe kuwa, wapo waliopewa dhamana ya kuongoza nchi hii wakipewa Ukurugenzi, Uwaziri na vyeo vingine na kujiangalia wenyewe badala ya kutumikia nchi na wananchi.

“Tatizo hili haliwezi kuisha, wananchi wataendelea kulalamika
kwa sababu wametanguliza ubinafsi mbele na kujinufaisha, ipo siku wataulizwa ulipewa Ukurugenzi na vyeo vingine kwanini kanisa linaangaika,” alisema Padri Magafu.

Katika uvamizi huo ambao ulifanyika saa tisa usiku, Bw. Fute alijeruhiwa kichwani, mguuni na mkononi baada ya purukushani
za kushinikizwa na watu hao awapeleke kwa Askofu Mokiwa.

No comments:

Post a Comment