11 March 2013

Maalim Seif ambana JK ripoti za mauaji



Peter Mwenda na Anneth Kagenda

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameitaka Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iweke hadharani matokeo ya uchunguzi wa matukio mbalimbali ya
mauaji na utekwaji nyara uliotokea hivi karibuni nchini.


Matukio hayo ni pamoja na lile la mauaji ya Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar aliyepigwa risasi na watu wasiofahamika hivi karibuni.

Bw. Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kigogo, Manispaa ya Kinondoni.

Alisema mara nyingi vifo vyenye utata vinapotokea, lawama huelekezwa kwa CUF kwamba ndicho kimechangia jambo ambalo haliona ukweli wowote hivyo ni muda muafaka kwa Rais Kikwete kuweka hadharani ripoti husika na mauaji yaliyotokea ili wananchi waweze kujua ukweli wa kile kinachozungumzwa.

“Namuomba Rais Kikwete apatapo ripoti za mauaji yenye utata, asiiweke ndani au kuisoma na watu wachache badala yake aitoe
kwa wananchi ili wajue wahusika ikiwemo ile ya mauaji ya Padri Mushi aliyeuawa Zanzibar hivi karibuni,” alisema.

Aliongeza kuwa, matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi baada ya vifo hivyo yanamshangaza hasa wanapoyahusisha na ugaidi ambapo kama waliwajua wahusika, kwanini wapeleke wapelelezi kutoka nje ya nchi.

“Viongozi chungeni kauli zetu...kama mtu aliyefanya tukio hilo anajulikana kwanini msimtaje badala yake mnateua tume za kuchunguza bila wananchi kupewa matokeo.

“Hadi leo tume iliyochunguza tukio la kutengwa na kupigwa Dkt. Steven Ulimboka hadi leo haijatoa majibu yoyote,” alisema na kuvitaka vyombo vya dola, kuheshimu mawazo ya wananchi ambayo wanayapeleka ili waweze kufanikisha kazi zao.

Alisema hivi karibuni yameibuka mambo mengi ya kutisha kinyume na ustarabu wa Kitanzania kutekana, kuteswa na kuuawa lakini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio yenye jukumu la kulinda raia na mali zao na kuhoji kwanini mambo hayo yanapotokea Serikali inakaa kimya.

Bw. Hamad alisema, CUF inalaani vikali unyama aliofanyiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Bw. Absalom Kibanda na kudai unyama aliofanyiwa hauwezi kuvumilika.

No comments:

Post a Comment