11 March 2013

Wasilisheni maombi wajumbe wa baraza-Warioba


Na Grace Ndossa

MWENYIKITI wa Tume ya mabadiliko ya Katiba Mpya Jaji Joseph Warioba amewataka wananchi wenye sifa za kuwa wajumbe wa mabaraza  ya katiba ya Wilaya na ambao wangependa kuwa wajumbe wa mabaraza hayo  kuwasilisha maombi yao kwa maofisa watendaji wa  vijiji au mitaa kuanzia kesho hadi  machi 20 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Jaji Warioba  alisema kuwa ili kuhakikisha  mchakato wa uundwaji na uendeshaji  wa mabaraza ya katiba  unaendeshwa kwa ufanisi tume imeandaa muongozio wa kusimamia mchakato huo.

Alisema kuwa muongozo uliondaliwa na kutolewa na tume,unaeleza sifa za mwananchi anayependa kuomba nafasi ya kuwa mjumbe wa baraza la katiba ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania  na mwenye umri wa miaka 18 au zaidi .

Pia alisema kuwa  mwananchi atakayeomba awe na uwezo wa  kusoma na kuandika, awe ni mkazi wa kudumnu wa kijiji. mtaa, awe ni mtu mwenye hekima, busara na uadilifu na mwenye uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.

"Kila mwananchi atakayeomba  anapaswa kuwasilisha nakala mbili za barua ya maombi, barua moja itabaki katika ofisi ya mtendaji na barua ya pili atabaki nayo mwombaji baada ya kutiwa saini na kugongwa muhuri kudhibitisha kuwa ombi lake limekubaliwa,"alisema Jaji Warioba.

Hata hivyo alisema kuwa baada ya muda wa kuwasilisha maombi kukamilika tume imeeleza  mwongozo wake kuwa majina ya waombaji wote yatapaswa kuwa katika sehemu zote za wazi na mbao za matangazo za ofisi za watendaji, mitaa na vijiji kuanzia machi 22 hadi 28 ili wananchi waweze kuyapitia na  kujiridhisha  kuwa maombi yao yamepokelewa.

 Alisema kuanzi machi 30 hadi Aprili 4 kutafanyika mikutano maalum ya mitaa  vijiji na shehia kwa Zanzibar ili kufanya uchaguzi na  vikao maalum vya maendeleo ya kata vitakavyofanyika April 5 hadi April 9 ili kuchagua wawakilishi wa kata.

ALisema kuwa tume inaomba wananchi na viongozi wote kuendesha  mikutano ya uundwaji wa mabaraza kwa amani na utulivu na kuzingatia muongozo ulitolewa na tume.

No comments:

Post a Comment