11 March 2013

Mchungaji mbaroni kwa kutorosha wanafunzi

 Na Heckton Chuwa,
Moshi

JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro,linamshikilia mtu mmoja anaedaiwa kuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,(DRC), kwa tuhuma ya kuwatorosha wanafunzi wawili, (majina yanahifadhiwa), kwa lengo la kuwasafirisha nje ya
nchi.


Akidhibitisha taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani
Kilimanjaro Kamishina Msaidizi wa Polisi, (ACP), Robert Boaz, alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Jean Felix, anaedaiwa kuwa Mchungaji anaefanya mahubiri
yake kwenye Kanisa moja Jijini Dar es Salaam.

“Mtuhumiwa huyu alikamatiwa Dar es Salaam na kusafirishwa kuletwa mkoani hapa jana, (Jumatano), kujibu tuhuma zinazomkabili kwa vile jalada lilifunguliwa katika Mkoa Kilimanjaro”, alisema.

Alisema taarifa za awali zinaonyesha ya kuwa aliwarubuni watoto hao ya kuwa anakwenda kuwatafutia vyuo nje ya nch, ambapo taarifa
zingine kutoka kwa raia wema zilionyesha ya kuwa alikuwa akiishi nao kwenye hoteli moja huko Jijini Dar es Salaam.

Akiongelea swala hilo kwa uchungu mjini Moshi jana,
(Alhamisi), mzazi wa watoto hao Bw. Maynard Swai, alisema watoto hao waliondoka Moshi Jumanne iliyopita na Mchungaji huyo alisema ni maarufu kama Pastor Jean.

Bw. Swai alisema yeye na wenzake wa nyumbani kwake walipata wasiwasi baada ya mmoja ya watoto hao kuacha barua iliyosema ya kuwa yeye na mdogo wake wasitafutwe kwa vile wamepata mfadhili atakaewatimizia ndoto zao za kimaisha.

“Bahati njema ni kuwa mmoja wa watoto hawa aliacha simu yake ya mkononi na tulipoichukua na kuanza kufuatilia mawasiliano aliyokuwa akiyafanya
tukagundua alikuwa akiwasiliana na mtu anaejiita Pastor Jean na ndipo nikashirikiana na jeshi la polisi kumfuatilia kwa kutumia namba yake ya simu”,
alisema.

Kwa mujibun wa Bw. Swai, baada ya muda namba ya Mchungaji huyo haikuwa inapatikana tena hewani na kwamba wakati akizungumzia swala hilo Jijini Dar es Salaam alipokwenda kuwafuatilia watoto hao, mmoja wa jamaa zake alimweleza ya kuwa anamfahamu Pastor huyo, lakini alipompigia pia hakumpata.

“Ndugu huyu aliwasiliana na Mchungaji Getrude Lwakatare ambapo tulimfuata na tulipofika na kumueleza Mch. Lwakatare aliwasiliana na
Jean na muda mfupi akatuhakikishia Pastor huyo atawaleta watoto pale Mikocheni tulipokuwa”, alisema.

Alisema baada ya muda watoto wale walifikishwa eneo la Mikocheni kwa teksi ingawa Pastor Jean mwenyewe hakuwepo na kwamba ilibidi atoe taarifa polisi na ndipo alipokamatwa akiwa hotelini.

“Cha kushangaza nilipowauliza wanangu wangesafiri vipi wakati hawakuwa na paspoti za kusafiria, wao walisema ya kuwa Pastor huyo alikuwa anasubiri paspoti zao kutoka DRC alikokuwa ameziagizia”, alisema.

Alisema watoto hao walimwambia ya kuwa Pastor huyo aliwaambia ya kuwa wasiwe na wasiwasi kwa vile yeye
anasomesha zaidi ya watoto 200 sehemu mbalimbali duniani na kwamba ana ofisi na makazi katika miji ya Johanesburg, Kinshasa, Paris na Lusaka.

“Pia aliwaambia wasifanye mawasiliano na mtu yeyote na kwamba kuanzia siku hiyo mawasiliano yote yatakuwa yanapitia kwake na kwamba wasiwajulishe wazazi wao kuhusu safari hiyo maana wazazi wa siku hizi si waelewa na kwamba watawaharibia mipango yao mizuri ya kujiendeleza kimaisha”,alisema.

Bw. Swai alitoa wito kwa mamlaka husika hapa nchini kuangalia uwezekano wa kulifuatilia kwa kina swala hilo haswa kutokana na hivi karibuni kuwepo kwa taarifa nyingi za kutoweka kwa watoto hapa nchini ambazo kila kukicha zinazidi kutangazwa.

“Kuna aina mpya ya ujangili wa kusafirisha binadamu haswa watoto wadogo na vijana kwenda nje ya nchi, wengine inadaiwa wanapelekwa kwenda kushiriki vita, wengine kwenye madanguro, hii ni hatari ni lazima hatua za haraka zichukuliwe”, alisema.

 

No comments:

Post a Comment