12 March 2013

Washtakiwa kesi ya uchochezi, wizi wakana waelezo ya awali


Rehema Mohamed na Rehema Maigala

WASHTAKIWA wa kesi ya wizi na uchochezi inamkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Issa Ponda na wenzake, jana waliendelea kujitetea baadhi yao wakikana maelezo ya awali waliyotoa katika Kituoa cha Polisi Mabatini, Kijitonyama.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wametoa utetezi wao kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Victoria Nongwa wakiongozwa na wakili wao, Bw.
Juma Nassoro.

Mshtakiwa Alawi Musa, alikana maelezo yake na kudai kuwa, alikwenda katika Msikiti wa Changombe Markaz, kwenye ibada
ya Itikafu kwa ajili ya kukomboa eneo la Waislamu lililouzwa.

Alawi alikana maelezo ya kuhusika kujenga Msikiti wa muda
katika eneo la Markaz, linalomilikiwa na Kampuni ya Agritanza
Ltd, wakati wakati akihojiwa na wakili wa Serikali Tumaini Kweka.

Katika maelezo aliyotoa polisi, mshtakiwa huyo alidai yeye ni mzaliwa wa Zanzibar, Kijiji cha Ole na alikuja Dar es Salaam mwaka 2008, lakini wakili huyo alipomuhoji kuhusu
maelezo hayo pia aliyakana.

Kwa upande wake, mshtakiwa Ramadhani Rashidi katika maelezo aliyotoa polisi, alidai kuwa yeye ni mkazi wa Mlandizi na alipata taarifa za kusaidia ujenzi wa Msikiti katika kiwanja cha Chang'ombe Markaz kutoka kwa imamu wake wa Msikiti wa Nuruh.

Katika maelezo hayo, alidaikuwa baada ya kupata taarifa hizo alikuja Dar es Salaam na kwenda Chang'ombe Markaz, Oktoba 15,2012 na walikamatwa na polisi Oktoba 16 mwaka huo usiku.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana maelezo hayo na kudai polisi walimuhoji jina lake, umri na anapoishi ambapo suala la kwenda Chang'ombe Markaz, kujenga msikiti halijui hivyo huenda polisi wamejiandikia.

Shekhe Ponda na wenzake wanakabiliwa na makosa matano
ambapo Oktoba 12 ,2012 wanadaiwa kula njama na kuvamia kiwanja kinachomilikiwa na Kampuni ya Agritaza Ltd
kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.

Katika kosa la uchochezi, inadaiwa Shekhe Ponda na Salehe Mkadam wakiwa katika eneo la Chang'ombe Markaz na viongozi
wa taasisi hiyo, waliwashawishi wafuasi wao ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo kutenda makosa hayo.

No comments:

Post a Comment