12 March 2013

DC Korogwe apinga taarifa ya Ofisa Elimu matokeo kidato IV


Na Yusuph Mussa, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, ameungana na vyama vya upinzani kuikataa taarifa ya Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wilayani humo Bw. Shabaan Shemzigwa, kuhusu chanzo cha kufeli kwa wanafunzi wa
kidato cha nne mwaka 2012 na kudai haina mashiko.


Akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), Kaimu Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF), wilayani humo, Bw. Ibrahim Abdillah, alisema taarifa hiyo haioneshi matatizo yaliyochangia wanafunzi kufanya vibaya zaidi.

“Mwenyekiti (DC), naomba tuikatae taarifa ya Ofisa Elimu kwani haioneshi tatizo lililofanya wanafunzi kufeli zaidi ya kuja na asilimia ya watoto waliopata sifuri, pia hawaoneshi ni jitihada gani ambazo  watafanya ili kumaliza tatizo hili,” alisema Bw. Abdillah.

Kwa upande wake, Bw. Shemzigwa alijitetea na kudai kuwa, alipata taarifa kikao hicho siku moja kabla hivyo ameshindwa kuingiza vitu vingi kwenye ripoti yake na kukiri kasoro hizo lakini alimtibua Bw. Gambo baada ya kusema kuwa, tatizo la kufeli ni la kitaifa.

Bw. Gambo alimwambia Bw. Shemzigwa kuwa, asilete taarifa ambazo zinazungumzia Taifa katika kikao hicho bali yeye anapaswa kusema ni nambna gani wataweza kumaliza tatizo la watoto kufeli wilayani humo.

“Taarifa iliyotolewa na Ofisa Elimu inaonesha kama funika kombe mwanaharamu apite, haioneshi mkakati au jitihada gani zitafanyika kupunguza matokeo mabaya kwa wanafunzi... taarifa hii ni sawa na utani, dharau na mazoea.

“Acha kusema wanafunzi kupata sifuri ni tatizo la Taifa, kwani mimi, mke wangu na mtoto wangu tumepata zero...zungumzia nini kifanyike ili kuondoa tatizo hili, kama ningekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ningemuandikia barua Ofisa Elimu ya kujieleza kwa nini asishushwe cheo,” alisema Bw. Gambo.

Aliongeza kuwa, anaungana mkono msimamo wa vyama vya upinzani kuikataa taarifa hiyo na kumtaka Bw. Shemzigwa aiondoe kwenye kumbukumbu za DCC na kuiwasilisha wakati ujao.

Alisema kama Watanzania tunataka ufaulu mzuri kwa watoto wao, wanapaswa kuacha kuingiza siasa na haki za binadamu kwenye masuala ya elimu kwani kuacha kuwachapa viboko wanafunzi kupunguza nidhamu shuleni ambayo ndio msingi wa mafanikio.

taarifa hiyo ilisema wanafunzi 1,727 waliomaliza kidato cha nne wilayani humo mwaka 2012, walipata sifuri sawa na asilimia 83.269.

Akizungumza na gazeti hili baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani humo, Dunstan Mdoe, alisema kuwe na masharti magumu kwa wakuu wa shule za sekondari kuwa atakayeshindwa kufikia
kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wake afukuzwe.

1 comment:

  1. TATIZO LA KUFELI WANAFUNZI NI KUSHUKA KWA ELIMU KWENYE NGAZI ZOTE NCHINI KUANZIA CHEKECHEA HADI CHUO KIKUU INATAKIWA TUME KUTOKA AU AU UNO ILIYO HURU IKACHUNGUZE ELIMU TANZANIA KABLA ,WAKATI NA BAADA YA UHURU WANAOTAKIWA KUHOJIWA NI WATANZANIA WA RIKA ZOTE WATAJICHUNGUZAJE

    ReplyDelete