11 March 2013

Wanafunzi kidato cha II wakimbia masomo


Na Masau Bwire, Rufiji

ZAIDI ya nusu ya wanafunzi waliofeli mtihani wa kidato cha pili mwaka 2012 na kutakiwa kurudia masomo mwaka huu katika Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, hawajaripoti shuleni na hawajulikani waliko.


Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Leo Rwegasira, alisema kati
ya wanafunzi 904 waliofeli mtihani huo mwak 2012, waliorudi shuleni na kuanza masomo ni 442.

Alisema sababu moja wapo iliyochangia washindwe kuripoti
shuleni na kuanza masomo ni aibu waliyonayo kwa wenzao
ambao wanaendelea na masomo baada ya kufaulu mtihani.

Aliongeza kuwa, sababu nyingine ni wazazi wa wanafunzi hao kushindwa kuwahamasisha na kuwahimiza waende shule wakiamini kuendelea kuwasomesha ni kupoteza muda, fedha na kufeli tena.

“Sababu nyingine ni mwamko mdogo wa elimu kwa wananchi
wengi ambao hawako tayari kuwasomesha watoto wao kwa hiari hivyo kufeli kwao ni jambo la faraja ili wakae nyumbani pamoja
na kufanya shughuli za kilimo,” alisema.

Hata hivyo, Bw. Rwegasira alisema, Serikali ya wilayani humo imewataka wanafunzi wote waliofeli mtihani huo, kuripoti shuleni ifikapo mwishoni mwa mwezi huu vinginevyo watasakwa,  kuchukuliwa hatua na wazazi wao kuwafikisha mahakamani.

Halmashauri hiyo ina shule 20 za sekondari ambazo kati ya hizo,
19 za Serikali na moja nya binafsi ambazo kwa ujumla wake, katika matokeo ya kidato cha pili 2012, wanafunzi 904 walifeli mtihani huo ambapo mfumo uliopo sasa, wanapaswa kurudia kidato masomo mwaka mzima na kurudia mtihani huo.

No comments:

Post a Comment