11 March 2013

DC ambana Mbunge wa Korogwe kuelezea kazi za Mfuko wa JimboNa Yusuph Mussa, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho
Gambo amemtaka mbunge wa Korogwe Mjini, Bw. Yusuph
Nassir, kuzunguka jimboni kwake ili kuwaeleza wananchi
kazi zinazofanywa na Mfuko wa Jimbo.

Alisema wananchi wengi jimboni humo wanalalamika na kudai
hawajui kazi zinazofanywa na mfuko huo tangu uanzishwe.

Bw. Gambo aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika Kikao
cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), kilichofanyika kwenye Halmashauri ya Mji wa Korogwe ambapo Kaimu Katibu wa
Chama cha Wananchi (CUF), wilayani humo Bw. Ibrhaim
Abdillah, naye alitaka kufahamu kazi za mfuko huo.

Alisema mfuko huo kwa wakazi wa Korogwe Mjini ni hadithi wanayoisikia kupitia majimbo mengine na Bw. Nassir hajafanya mkutano wowote wa hadhara, mtaa au kijiji ili kuzungumzia kazi zinazofanywa au zilizofanywa na mfuko husika.

Aliongeza kuwa, wananchi hawafahamu Mfuko wa Jimbo ni kitu gani na matumizi yake ni yapi hivyo wananchi wameachwa njia panda bila kujua kinachoendelea kuhusu mfuko huo.

“Nitamuagiza Katibu wa DCC amuandikie barua mbunge wa Korogwe Mjini ili aweze kufanya mikutano na wananchi wake
kuwaeleza kazi za Mfuko wa Jimbo kama anavyofanya mwenzake Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani 'Majimarefu'.

“Bw. Ngonyani kila anapofanya mkutano kwenye kata na vijiji vilivyopo jimboni kwake, anawaeleza wananchi kazi alizozifanya kupitia Mfuko wa Jimbo, Serikali Kuu na miradi aliyoifanikisha kupitia fedha zake za mfukoni,” alisema Bw. Gambo.

Kaimu Mwenyekiti wa CUF, wilayani humo, Bw. Salum Jabu, alimuunga mkono Bw. Gambo na kusema kuwa, kazi zilizofanywa na Bw. Ngonyani kupitia mfuko wa jimbo na zile anazofanya kupitia fedha zake za mfukoni anazitangaza kwenye mikutano yake,

Bw. Jabu alisema, Bw. Ngonyani amenunua jenereta lenye thamani ya sh. milioni tano kwa fedha zake za mfukoni kwa ajili ya Kituo cha Afya Mombo ili upasuaji usiweze kukwama pamoja na kusaidia ujenzi wa choo cha Soko la Mombo.

No comments:

Post a Comment