18 March 2013
Vijana watakiwa kuacha propaganda,wachape kazi
Na Florah Temba,
Moshi.
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Kilimanjaro,umewataka vijana wa chama hicho kufanya kazi na kuacha propaganda, hatua ambayo itakiwezesha chama cha CCM kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika mwakani 2014, na kuyakomboa majimbo yaliyochukuliwa na upinzani katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa umoja huo mkoani hapa, Bw. Frederick Mushi, wakati akifungua kikao cha kawaida cha baraza la vijana mkoa wa
Kilimanjaro, kilichofanyika mjini Moshi na kuhudhuriwa na wajumbe 40 wa baraza hilo.
Bw. Mushi alisema wananchi kwa sasa wanahitaji kazi na si Propaganda, hivyo ni vema vijana wakajipanga vizuri ili kuhakikisha chama hicho kinashinda
katika maeneo mbalimbali kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.
"Tunaingia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani,tuanze kujipanga kuanzia sasa sisi kama vijana, kwani hatuwezi kushinda kwa kusema CCM hoye
na kunyoosha vidole gumba, ni lazima tujipange na kuweka mikakati,"alisema.
Naye Katibu wa UVCCM mkoani hapa Bw. Yasin Lema, aliwataka vijana kuungana kufanya kazi kwa umoja na mshikamano na kuepuka makundi ambayo yanayoweza kuwavuruga katika umoja wao.
Kwa Upande wake Katibu CCM mkoani Kilimanjaro Bw. Steven Kazidi, aliwataka vijana kubadilika na kujitambua, hatua ambayo itawawezesha kupiga hatua katika mikakati mbalimbali ya kimaendeleo.
Katibu huyo aliwataka pia vijana kuepuka kutumiwa na watu wachache kwa maslahi binafsi kutokana na kwamba kufanya hivyo kunaweza kuwayumbisha katika nafasi zao na kuwafanya washindwe kutekeleza vema majukumu yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment