18 March 2013

Mkuchika azungumzia vurugu za wanasiasa Masasi



Na Casmir Ndambalilo, Masasi

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika, amekemea vurugu zinazoanzishwa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati nchini ili kujipatia umaarufu kwa kuwapotosha wananchi juu ya uendeshwaji wa Serikali iliyoko madarakani inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Bw.Mkuchika aliyasema hayo jana katika Wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Yatima, akiwa katika ziara ya kuwapa pole wahanga wa vurugu zilizotokea hivi karibuni.

Katika vurugu hizo, watu wanne wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya, mali za umma, watu binafsi kuharibiwa.

Akihutubia umati wa watu bila kujali mvua iliyokuwa ikinyesha, Bw. Mkuchika aliwataka viongozi wa chama na Serikali wilayani humo kuacha woga wa kuelezea maamuzi yanayotolewa na Serikali Kuu juu ya mipango ya maendeleo kwa wananchi nchini.

Alisema Serikali ya CCM ndiyo iliyoshika dola hivyo kuacha vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu vikiendelea ni sawa na kusalimu amri na kuifanya nchi isitawalike.

Amewataka viongozi wa Serikali na chama, kutoruhusu hali hiyo itokee kwani athari zake ni kubwa.

“Watu wanakuja hapa na kuhamasisha vijana wenu kufanya vurugu na maandamano mnawaangalia tu, nimesikitishwa sana na hali kama hii kwani wananchi wa Wilaya hii na nyingine za Mkoa huu hawana utamaduni wa kuandamana au kufanya vurugu.

“Lazima viongozi wa Serikali na chama muhakikishe mnatoa elimu kwa wananchi mara kwa mara juu ya maamuzi yanayofanywa na Serikali ili waelewe, jambo ambalo litawafanya waunge mkono
na kushirikiana katika kutekeleza,” alisema.

Aliongeza kuwa, baada ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupata taarifa ya matukio ya vurugu zilizotokea Masasi na Mtwara Mjini, imetoa tamko la kusisitiza kupeleka gesi Dar es Salaam kwani hakutaathiri maaendeleo ya wananchi wa Mkoa huo.

Bw. Mkuchika alisema tamko hilo limesisitiza pamoja na mambo mengine, kuwataka viongozi wa chama na Serikali mkoani humo kutoa elimu inayohusu suala la gesi.

“Kutokana na kuwepo kwa gesi nyingi mkoani Mtwara, Serikali imeamua kupeleka gesi asilimia 16 tu jijini Dar es Salaam ambapo asilimia 84 inayobaki, inatosheleza matumizi ya wakazi wa Mkoa huu kwa matumizi ya umeme wa majumbani na viwanda.

“Visima vya gesi vinne vimegunduliwa kuwa na gesi, hadi sasa ni kimoja tu kinachochimbwa na gesi inayotolewa haifiki hata
asilimia moja,” alisema Bw. Mkuchika.

Alisema wananchi wa Mtwara Mjini, Vijijini, Tandahimba, Newala na Masasi, hivi sasa wanafaidika na gesi hiyo kwa kuunganishiwa umeme ambapo Wilaya ya Nanyumbu, nayo inatarajiwa kupata umeme unaotokana na gesi hiyo hivi karibuni.

Aliongeza kuwa, Mkoa huo utafaidika na gesi hiyo kutokana na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Saruji Dangote ambacho tayari mkandarasi yupo kazini na kiwanda cha mbolea ambapo ujenzi huo, tayari unawanufaisha vijana wanaofanya kazi.

Alisema gesi inayopatikana Mtwara ni rasilimali ya Taifa kama zilivyo nyingine katika mikoa mbalimbali nchini kama madini yanayochimbwa Mikoa ya Arusha, Mwanza, Shinyanga ambapo fedha zinazopatikana, hutumika kununulia dawa na huduma nyingine za kijamii bila kubagua Mkoa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Masasi, Kazumari Kazumari Malilo, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Farida Mgomi, alisema uongozi wilayani humo uliduwazwa na vurugu zilizotokea na kushindwa uanzie wapi kuwaweka sawa wananchi.

No comments:

Post a Comment