18 March 2013
Ajeruhiwa vibaya na mamba wakati akichota maji mtoni
Na Joseph Mwambije,Namtumbo
MKAZI mmoja wa kijiji cha Likuyu wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Bw.Rashid Almasi(59)amejeruhiwa vibaya na mamba baada ya kupambana na mamba huyo na hatimaye kumshinda nguvu.
Akizungumza na gazeti hili jana katika Hospitali ya Mkoa wa Songea (HOMSO) alikolazwa majeruhi
huyo Rashid Almasi alisema kuwa mkasa huo ulimkuta wakati akienda kuchota maji ya kunywa katika mto wa Likuyu.
Bw.Almasi alisema kuwa alipokuwa akichota maji katika mto huo ghafla alikutwa anakamatwa na mnyama
huyo ndipo alipoanza kupambana naye huku akikumbuka kuwa ana kisu ambacho kilimsaidia katika mapambano hayo ambayo yalimfanya mnyama huyo kukimbia na
kumuacha akiwa amejeruhiwa vibaya.
"Nilipochukua kisu na kumchoma mamba huyo alikuwa hataki kuniachia lakini nilipozidi kuongeza kasi ya
mapambano kwa kumchoma sehemu mbalimbali za mwili mnyama huyo ndipo alipo niachia na kuzama kwenye maji,"alisema
Alisema kuwa alipofanikiwa kutoka katika mapambano hayo alijiangalia sehemu ya tumbo lake na kuona utumbo wake umetoka nje, ambapo alidai kushtuka, lakini alijitahidi kuakikisha kwamba utumbo huo haupati mchanga
"Nilipiga kelele za kuomba msaada kwa wasamaria wema wakajitokeza na kunipatia huduma ya kwanza, ambapo watu wanaofanya kazi katika HIfadhi ya Selous walitoa gari lao na kumkimbiza katika hospitali ya Songea,"alisema.
Alisema kuwa kwa sasa anaendelea baada ya kupatiwa matibabu, tofauti na ilivyokuwa awali,kwani hali yake ilikuwa mbaya kabla ya kupatiwa matibabu.
Kwa upande wake Dkt.Mathayo Chanangula alisema kuwa mgonjwa huyo alipokelewa hapo Machi 7 mwaka huu, ambapo alipewa huduma ya kupelekwa chumba cha
upasuaji, ambako walibaini utumbo ulikuwa ukibembea nje hivyo umerudishwa mahali pake na sasa anaendelea vizuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment