19 March 2013

Utumishi yaonya matangazo feki ya ajira



Na Peter Mwenda

SEKRETARIETI ya Ajira imeonya kuwa wao pekee ndiyo wenye jukumu la kutoa matangazo mbalimbali yanayohusiana na mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais,Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa vyombo vya habari jana Dar es Salaam ilisema kuwa matangazo yanayochapishwa au kuandikwa katika mitandao ya kijamii hazijatolewa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.


"Kutokana na maelezo hayo hapo juu ni vyema wananchi wote wakafahamu kuwa ni kosa kwa mtu au taasisi yeyote ile kuchukua matangazo kwa lengo la kupotosha umma ilihali wakijua wazi kuwa taarifa hizo zinapaswa kutolewa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma,"ilisema taarifa hiyo.

Ilisema Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1) na kuongeza kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma limetokana na maboresho yanayoendelea katika Utumishi wa Umma nchini.

Miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na marekebisho ya Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 toleo Na. 2 la mwaka 2008 ambapo katika Vifungu Na. 4.6  na 6.6. vya Sera hiyo ambavyo vimetamka kuwepo kwa chombo maalum cha kushughulikia ajira katika Utumishi wa Umma.

Taarifa hiyo ilisema kwa mujibu wa Sheria, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ndio chombo pekee chenye wajibu wa kutekeleza  majukumu ya kutafuta wataalam wenye ujuzi maalum na kuandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za wataalam na kutangaza nafasi wazi za kazi zinazojitokeza katika Utumishi wa Umma.

Iliendelea kuwa inahusisha wataalam maalum ili kushirikiana nao kwa ajili ya kufanya usaili kulingana na mahitaji, kuwashauri waajiri kuhusu masuala yanayohusiana na mchakato wa ajira na kuandaa orodha ya wahitimu wa vyuo na wataalam weledi kwa madhumuni ya kurahisisha rejea za ujazaji wa nafasi za ajira katika Utumishi wa Umma.

Ilisema kwa mujibu wa sera hiyo, kuwepo kwa chombo hiki kutaziwezesha Mamlaka za Ajira nchini zikiwemo za Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa kubaki na majukumu yake ya msingi ambayo yameainishwa katika uundaji wa mamlaka hizo ili kuongeza ufanisi. 

Taarifa hiyo pia ilisema wamefikia hatua ya kusema hayo kutokana na baadhi ya taarifa zinazohusu mchakato wa ajira hususani uwepo wa nafasi za kazi zilizopo katika baadhi ya mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira ametoa matangazo hayo.

Ilisema moja ya tangazo hilo la kughushi na lenye nia ya kupotosha umma ni lile lililoko katika anwani ya www.eastafricajobscareer.com lenye kichwa cha habari kinachosomeka “Tangazo la Kazi Utumishi Tanzania Juni 2013” ambalo linaonyesha “Mwisho wa kupokea barua za maombi ni Juni 8, 2013”.

Pia iliongeza kuwa wadau wote wa Sekretarieti ya Ajira wanaotafuta kazi pindi wanapoona matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari wajiridhishe kwa kuthibitisha taarifa hizo kama ni za kweli kwa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz kwa taarifa sahihi zinazohusu ajira katika Utumishi wa Umma.

No comments:

Post a Comment