19 March 2013

Trafiki agongwa, afa akiwa kazini Dar


Na Waandishi Wetu

ASKARI wa Kitengo cha Usalama Barabarani, WP 2492 Elikiza Nko, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari yenye namba 
T 328 BML, aina ya Land Rover Discover, mali ya Kanisa la
TAG wakati akiongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete.

Tukio hilo lilitokea Dar es salaam jana, saa saba mchana eneo la Bamaga, Mwenge wakati askari huyo akiongoza magari mara
baada ya msafara huo kupita.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

“Askari huu alifariki akiwa kazini wakti akiongoza magari, baada
ya msafara wa Rais Kikwete kupita eneo lake, aliendelea kuruhusu magari kutoka Barabara ya Shekilango ndipo dereva wa gari iliyosababisha ajali, akitokea Sayansi kwenda Mwenge,
alimgonga na kufa papo hapo,” alisema.

Kamanda Kenyela alisema, kuwa dereva wa gari hilo alikimbia
baada ya tukio na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Hata hivyo, Kamanda Kenyela ametoa onyo kwa madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani kuacha tabia hiyo
na kuwataka wananchi watoe ushirikiano kwa jeshi hilo ili kufanikisha kukamatwa kwa madereva wa aina hiyo.


Aliongeza kuwa, ajali hiyo ni changamoto kubwa kwa jeshi hilo Kikosi cha Usalama Barabarani.

No comments:

Post a Comment