19 March 2013

Marekani kupambana na rushwa nchini



Na Godfrey Ismaely

BALOZI wa Marekani nchini, Bw. Alfonso Lenhardt, amesema kuanzia sasa Serikali yake itashiriki kikamilifu kupambana na rushwa nchini hasa kwa viongozi.


Alisema ili kufanikisha azma hiyo, nchi yake itashirikiana na Jaji Othman Chande wa Tanzania, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rusha nchini (TAKUKURU), chini ya Mkurugenzi wake, Dkt. Edward Hosea, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), ili kuhakikisha tatizo la rushwa linaisha.

Balozi Lenhardt aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kikao maalumu cha waandishi wa habari, ambacho kiliandaliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Katika kikao hicho, Gazeti la Majira lilitaka kufahamu jinsi Serikali ya Marekani ilivyojipanga ili kurejesha uwajibikaji na uwazi kwa viongozi mbalimbali nchini ambao wanazorotesha miradi ya maendeleo ukiwemo ushiriki wao katika midahalo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Alisema ni alama mbaya kwa Taifa la Tanzania kukithiri vitendo vya rushwa akitolea mfano kwenye Jeshi la Polisi na hospitalini.

“Ufike wakati Watanzania tuseme basi, kama unaendesha gari na umefanya makosa, polisi akija akitaka fedha usimpe, chukua jina lake na namba kisha mwambie akuandikie risiti ya kosa lako
uende ukalipie mahala husika, kisha mripoti Makao Makuu.

“Rushwa ipo kila sehemu si Tanzania pekee ila kinachotakiwa
ni kusema basi kwani inashangaza hata hospitalini mtu akitaka kukuhudumia hadi umpe fedha...usikubali sema rushwa basi,” alisema Balozi  Lenhardt.

Akizungumza kuhusu USAID jinsi inavyodanya kazi nchini, Balozi  Lenhardt alisema, “Tunaloangalia ni jinsi mpango huu unavyogusa maisha ya Watanzania katika utekelezaji wake ambapo mwaka 2012, tulichangia zaidi ya dola za Marekani milioni 700 (zaidi ya shilingi trilioni moja za Kitanzania).

Alisema fedha hizo ni msaada rasmi wa kiserikali kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na watu wa Marekani.

Naye Mkurugenzi mpya wa USAID, Bi. Sharon Cromer alisema shirika hilo limejipanga kuhakikisha linasaidia masuala ya kilimo,
afya, kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kupambana na malaria.
Kupitia mpango wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na ugonjwa huo (PMI).

No comments:

Post a Comment