13 March 2013

TCRA: Mionzi ya simu haina madhara


Na Darlin Said

MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA), imekanusha taarifa zinazodai mionzi inayotumika katika vyombo vya mawasiliano ikiwemo simu za mkononi, ina madhara kwa afya ya binadamu.


Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma, aliyasema
hayo Dar es Salaama jana katika warsha ambayo iliandaliwa kwa waandishi wa habari kuhusu mambo ya mionzi na matumizi yake katika jamii.

Alisema tafiti zilizofanywa nchini hivi karibuni, zimeonesha
hakuna madhara yeyote yanayosababishwa na mionzi ambayo inatokana na minara ya vyombo vya mawasiliano.

Aliviomba vyombo vya habari nchini, kutoa elimu kwa jamii ili kuwaondoa hofu wananchi waendelee kuvitumia vyombo hivyo zikiwemo simu za mkononi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu ya Atomic nchini (TAEC), Bw. Mwisarubi Nyaruba, alisema mionzi imegawanyika katika makundi mawili ambayo yametofautishwa kulingana na viwango vya kimataifa.

“Lipo kundi lenye kiwango kikubwa cha mionzi ambayo hutumika sana katika shughuli za hospitalini, kilimo, barabara na viwandani wakati kundi lingine lina kiwango kidogo na mionzi yake haina nguvu ambayo hutumika katika vyombo vya mawasiliano
zikiwemo simu za mkononi,” alisema.

Bw. Nyaruba aliongeza kuwa, vyombo vya mawasilano vinatumia kiwango kidogo cha mionziambayo haiwezi kuleta madhara kwa binadamu.

Wakati huo huo, Prof. Nkoma alisema TCRA haitasitisha mpango wa matumizi ya mfumo mpya wa digitali ambao umeanza rasmi Januari mosi mwaka huu, katika baadhi ya mikoa nchini.

Juzi Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), waliiomba Serikali kuangalia namna ya kuurudisha mfumo wa analojia uende sambamba na digitali ili  wananchi wapate muda
wa kujiandaa na mfumo mpya ambao umeonekana kuwaathiri
sana panmoja na vyombo vya utangazaji.

No comments:

Post a Comment