04 March 2013

Shibuda 'awalipua' viongozi wa CCM


Na Suleiman Abeid, Maswa

MBUNGE wa Maswa Magharibi, mkoani Simiyu, Bw. John Shibuda (CHADEMA), amekebea tabia ya baadhi ya viongozi
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayi humi wanaolitumia vibaya jina la Rais Jakaya Kikwete kuwatisha watendaji wa
Serikali.

Bw. Shibuda aliyasema hayo juzi mjini humo katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CHADEMA, ambao ulihudhuriwa na viongozi wa chama hicho mkoani humo, Mara na Shinyanga.

Alisema wapo baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM wilayani humo ambao wanawatisha watendaji wa Serikali na kudai kama hawatafuata matakwa yao, watamwambia Rais Kikwete
awahamisha vituo vya kazi mara moja.

“Hawa viongozi wanajifanya Rais Kikwete ni rafiki yao wa karibu ndio maana wanamtisha Mkuu wa Wilaya hii (Luteni mstaafu Abdalah Kihato), ambaye hivi karibuni alitoa amri ya kukamatwa mmoja wa viongozi wa CCM wilayani Bariadi.

“Kiongozi huyu alikamatwa kwenye mnada wa Maswa akiuza mahindi yaliyotolewa na Serikali kuwasaidia wananchi wenye
njaa, viongozi hawa ni waongo, hawana urafiki wowote na Rais Kikwete zaidi ya kumuona katika ziara na kwenye televisheni,” alisema Bw. Shibuda.

Alisema hayupo tayari kuona watendaji wa Serikali wakitishwa
na kushindwa kufanya kazi zao ipasavyo hivyo atamweleza Rais Kikwete mambo wanayofanyiwa wasaidizi wake.

Bw. Shibuda alimpongeza Bw. Kihato kwa ujasiri aliouonesha kutokana na agizo alilotoa la kukamatwa kiongozi wa CCM baada ya kubainika mahindi aliyokuwa akiyauza mnadani yaliyotolewa na Serikali kwa ajili ya wananchi wanaokabiliwa na njaa.

Pamoja na pongezi hizo, Bw. Shibuda alimuomba Rais Kikwete aitupie macho Wilaya hiyo kwani haina viongozi wa CCM ambao
ni waadilifu bali kuna kundi la watu waojali matumbo yao.

No comments:

Post a Comment