04 March 2013

Mganga wa kienyeji azua 'kizaazaa'



Na Steven William, Muheza

KUNDI la wakazi waishio Kijiji cha Kibanda, Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, juzi waliandamana hadi katika Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kushinikiza mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa jina la Aweso Kipaku, apewe kibali cha kuwasaka na kuwafichua wachawi waliopo kijijini hapo.

Mandamano hayo yalitawanywa na polisi kabla hayajafika
katika Ofisi ya Utamaduni wilayani humo.

Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw.
Salimu Mngia, alisema wakazi wa kijiji hicho tayari walichanga
fedha na kumpa mnganga huyo ili aweze kuifanya kazi hiyo.

Alisema baada ya kuchanga fedha hizo, walifanya taratibu
zote kwa Serikali ya kijiji ili kuridhia kazi hiyo pamoja na kuorodhesha majina ya watu ambao wangependa mganga
huyo aingie katika nyumba zao.

“Jambo la kushangaza, nimekuwa nikipigiwa simu na polisi
waliodai katika kijiji changu kuna uvunjifu wa amani na chanzo
cha maandamano ni baada ya mganga huyu kunyimwa kibali 
hivyo kilio chao ni kushinikiza aruhusiwe kufanya kazi.


“Jeshi la Polisi na Ofisi ya Utamaduni wanasema hawawezi
kutoa kibali kwa wakihofia uvunjifu wa amani,” alisema.

Kwa upande wake, Ofisa Utamaduni wilayani humo, Bw. Athumani Komolanya, alisema sheria zilizopo zinakataza mganga wa kienyeji kupita kila nyumba bali anapaswa kuwa katika eneo au nyumba moja na watu kumfuata mahali alipo.

Aliongeza kuwa, hawezio kutoa kibali kwani tayari suala hilo limeingia katika vyombo vya usalama na kuwataka wakazi hao
wakutane tena, kuandika ajenda na kuomba kibali upya.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Yambazi Semsanga, alikubaliana na ushauri uliotolewa na Bw. Komolanya
ambao watakwenda kuufanyia kazi.

No comments:

Post a Comment